Gilbert Bor anasimamia shamba dogo katika nyanda za juu za magharibi mwa Kenya. Ardhi ina vilima vingi na barabara za vijiji zimezingirwa na miti ya misonobali. Ng'ombe wake wengi ni wa uzao wa Friesian. Huwa anaamka saa 12:00 asubuhi kila siku kuelekeza wanyama wake kupitia misitu kwenye bonde la chini.
Wakulima wengi ndani na karibu na kijiji chake huko Kapseret wanapanda mahindi au maharagwe ili kujikimu. Lakini hili litabadilika, anasema Bwana Bor.
Mamlaka ya eneo la Afrika Mashariki imeanza kupendekeza ukuzaji wa mazao ya biashara kama parachichi na kahawa ili kuongeza mauzo ya nje ya Kenya kwa Umoja wa Ulaya na Uchina. Wakati huo huo, wakulima wa ndani wanajipanga pia, anasema Bwana Bor. Jamii yake mwenyewe iliwekeza kwa pamoja kwenye tangi la maziwa ili kuimarisha nafasi yake kwenye masoko ya maziwa ya kikanda.
"Kwa bidhaa kama kahawa, maembe au njugu, Ulaya ni soko muhimu," Bwana Bor anaeleza, kwa makini. “Mazao yanayouzwa nje kutoka Kenya yameondolewa ushuru huko Ulaya. Vivyo hivyo pia kwa mauzo ya nje kwenda Ulaya kutoka Ghana, Nijeria na nchi zinazozungumza Kifaransa. ”
Umoja wa Ulaya ni mbabe wa kilimo ulimwenguni. Jumuiya hii ya nchi 27 inapeleka msururu thabiti wa vyakula vilivyotayarishwa, nafaka, maziwa na nyama kwenye soko la ulimwengu huku ikiagiza bidhaa nyingi mbichi kama soya, miwa au mafuta ya mawese, mboga za kitropiki na matunda kama parachichi.
Kuwa makini kuhusu sera za Umoja wa Ulaya
Utandawazi unafanya masoko kupatikana kwa wakulima kama Bwana Bor. Anasema: ''Takriban nchi zote za Umoja wa Ulaya hununua bidhaa za kilimo kutoka Kenya. Maamuzi ya nchi kama Ujerumani au Uholanzi yatapambanua watakaonufaika zaidai. Wakulima wa Kiafrika lazima wawe makini kwa wanalofanya watunga sera wa Umoja wa Ulaya''
Hasa, wakulima wa Kiafrika wanahitaji kumakinikia mabadiliko ya Sera ya Pamoja ya Kilimo ya Umoja wa Ulaya (CAP) ambayo ilitungwa mnamo 1962 ili kutoa chakula cha bei nafuu kwa watu wake baada ya Vita vya Pili vya Kidunia.
Chini ya CAP, Umoja wa Ulaya ulifanikiwa pakubwa hivi kwamba kulikuwa na uzalishaji wa ziada. Baadaye mamlaka ilianzisha urejeshwaji wa fedha za—kuwalipa wafanyabiashara wa kimataifa tofauti kati ya bei za juu za ndani za Umoja wa Ulaya na bei ya chini ya soko la ulimwengu.
Ruzuku hizi zinaweka shinikizo kwa bei ya chakula ulimwenguni, na kusababisha athari mbaya kwa uchumi wa kilimo wa Kiafrika.
Hata hivyo, Umoja wa Ulaya ulisimamisha ruzuku zake za kupotosha biashara mnamo 2017. Mwaka mmoja baadaye Bunge la Umoja wa Ulaya, kwa mara ya kwanza kabisa, liliagiza utafiti kuhusu athari za CAP kote ulimwenguni.
"Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia maendeleo katika kusawazisha kilimo na malengo ya maendeleo ya kimataifa," anasema Maria Blanco, mwandishi mkuu wa Chuo Kikuu cha Ufundi huko Madrid, Uhispania.
Hata hivyo, kuongeza tu biashara ya kimataifa kwa bidhaa za kilimo hakuwezi kusababisha mapato bora moja kwa moja kwa wakulima wa Kiafrika, wataalam wanasema.
Zisipodhibitiwa, biashara kama hizi zinaweza kusababisha uharibifu wa mazingira, kuhamishwa kwa watu ndani ya nchi au ukiukwaji wa haki za binadamu.
Bi. Blanco anaonya: "Kuagiza miwa kutoka nje ya Ulaya kunaweza kujenga shughuli za kiuchumi kwa mataifa yanayoendelea. Lakini uagizaji wa bidhaa kutoka nchi zinazoendelea pia unaweza kusababisha unyakuzi wa ardhi au uchafuzi wa mazingira. ”
Kwa kawaida, bidhaa hupandwa kwenye mashamba makubwa. Mara tu pesa zinapoanza kumiminika, tamaa ya kiuchumi na kisiasa, huibushwa, na kuwaweka wakulima wadogo katika hatari. Mgeuko kuelekea mtindo wa kilimo cha viwandani huweka shinikizo kubwa kwa mazingira likija kwa suala la matumizi ya kemikali, ukataji miti au uchafuzi wa maji.
Shinikizo kutoka kwa mauzo ya nje
Utafiti uliofanywa na thinktank ARC2020 na Shirika lisilo la kiserikali kutoka Ujerumani Heinrich Böll Stiftung uligundua kuwa sera ya kilimo ya Umoja wa Ulaya inasababisha athari kubwa ulimwenguni kote. Mipangilio ya biashara, kwa mfano, Honduras ililimbikiza biashara ya ndizi kwa mashirika machache ya kimataifa huku mahitaji ya nafaka na soya huko Uropa yakihimiza udhibiti wa ardhi katika Asia ya Kati.
Licha ya mtazamo chanya, wakulima wa Kiafrika wako chini ya shinikizo lisilokoma la mauzo ya nje kutoka Umoja wa Ulaya. Baada ya masoko ya ndani ya Ulaya kujaa maziwa kufuatia jumuiya hiyo kuacha mfumo wake wa upendeleo mnamo 2015, wazalishaji wa Uholanzi na Wajerumani walitafuta haraka fursa zingine za kuuza nje.
Wahusika wa biashara ya maziwa ulimwenguni kama Danone au FrieslandCampina wameongeza uwezo wao wa uzalishaji katika Afrika Magharibi. Kampuni tanzu ya FrieslandCampina, WAMCO, inadhibiti zaidi ya asilimia 75 ya soko la maziwa nchini Nijeria.
Nchini Ghana, kuongezeka kwa ununuzi wa kuku waliogandishwa, kutoka tani 13,000 kwa mwaka 2003 hadi 175,000 mnamo 2019, kimeathiri uzalishaji wa ndani.
Zaidi ya asilimia 90 ya nyama ya kuku katika maduka makubwa nchini Ghana huletwa kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya.
“Kuku wana mauzo mengi na muda wake wa uzalishaji ni mfupi na hivyo waweza kukuza mapato kwa wafugaji nchini Ghana. Lakini mauzo ya kutoka nje ya kuku waliogandishwa huathiri vibaya sekta yetu ya nyama, ” Anthony Akunzule, mfugaji wa kuku analalamika.
Eneo Huru la Biashara Afrika
Eneo jipya la Biashara Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) linaweza kuimarisha juhudi za wakulima wa Kiafrika kushindana na Umoja wa Ulaya. Makubaliano ya biashara, yanayouondoa ushuru kati ya nchi za Kiafrika kwa asilimia 90 na kukabiliana na ucheleweshaji wa forodha ni mambo yanayoweza kukuza biashara ya kilimo ndani ya Afrika.
Profesa wa Sera ya Kilimo ya Ulaya Alan Matthews wa Chuo cha Trinity, Dublin, anasema mtazamo unageuka kutoka dhana kuwa CAP peke yake ndiyo inayohusika katika matatizo ya kilimo barani Afrika.
Bwana Mathews anasema kwamba serikali za Kiafrika zilishindwa kuweka kipaumbele kwa uwekezaji katika maeneo ya vijijini, huku wataalam wengi sasa wakiamini AfCFTA itabadilisha maendeleo ya Afrika.
Kile ambacho wakulima wa Afrika wanahitaji ni sera na hatua bora barani Afrika na Ulaya, anasema Bw. Bor. Kwa sasa, anasema kuwa, "Fursa zote zimewazingira wakulima wadogo kama mimi, hasa katika ukulima wa mazao ya kiasili."