Kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za mapema

Get monthly
e-newsletter

Kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za mapema

— Majadiliano na Mke wa Rais wa Sierra Leone, Fatima Maada Bio
Jocelyne Sambira
Afrika Upya: 
24 Novemba 2023
Majadiliano na Mke wa Rais wa Sierra Leone, Fatima Maada Bio.

Katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliokamilika hivi punde (UNGA78), Bi. Fatima Maada Bio, Mke wa Rais wa Sierra Leone alishiriki kikamilifu katika msururu wa matukio ya uwezeshaji wa kijinsia. Ushiriki wake unakusudia kuendeleza juhudi zake za kuimarisha haki za wanawake na kutetea hatua za kupambana na ubakaji na ndoa za mapema, katika nchi yake. Katika mahojiano na Jocelyn Sambira kutoka Afrika Upya, Bi Bio alifafanua masuala haya kwa kina. Haya hapa ni madondoo:

Umehudhuria matukio mengi ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Je, unaweza kuelezeaje tajriba yako mwaka huu?

Nilipohudhuria UNGA kwa mara ya kwanza mwaka wa 2018, nilikuja kujitambulisha na kuwafahamisha watu kuhusu kazi niliyokusudia kuifanya. Nilitaka kupata uungwaji mkono kadiri niwezavyo kwa sababu, linapokuja katika suala la jinsia, ushirikiano zaidi ya nchi moja ni muhimu.

Sasa, miaka mitano baadaye, naamini nimeunda ushirikiano wa kutegemewa. Nina watu binafsi ambao wanakubali utetezi wangu na kile ambacho nimekuwa nikitetea. Nadhani uthibitisho huu umekuwa muhimu sana kwangu - sihitaji tena kujitambulisha.

Je, nini kinachochochea hamu ya kutaka kupambana na unyanyasaji wa kijinsia?

Hatuwezi kujadili usawa wa kijinsia huku unyanyasaji wa kijinsia ungalipo. Vivyo hivyo, hatuwezi kujadili watoto na unyanyasaji kwa wakati mmoja. Hili ndilo limechochea hamu yangu, pamoja na kuwahi kupitia unyanyasaji mimi mwenyewe. Hii ndiyo sababu nililazimika kuvunja kimya changu. Wanawake wengi na wasichana wadogo husalia kimya, sio kwa sababu wanataka, lakini kwa sababu wanaamini hakuna mtu atakayesikia sauti zao.

Je, unahisi kuwa kuna mabadiliko katika mitazamo kuhusu usawa wa kijinsia?

Sasa tuna watu wengi wanaosikiliza, na wanaume wengi wanaanza kuelewa shida yetu. Nchini Sierra Leone, mawazo yetu yamebadilika kutoka kukubali hali ilivyo na kuanza kusema, "La, tunakataza jambo hili kuendelea katika nchi yetu." Wanawake wengi ambao wamefanya kazi zinazohusiana na suala hili sasa wanaamini kuwa tunaweza kukomesha unyanyasaji - na aina zote za dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana.

Je, mafunzo yapi unaweza kushiriki na nchi zingine? Kwa mfano, tunawezaje kuwalinda wanawake wakati wa migogoro?

Kwanza kabisa, paza sauti! Kimya hakijawahi kutatua matatizo yetu. Heshima yako tayari imevunjwa, imechukuliwa kutoka kwako. Jiambie mwenyewe na wengine, "Nataka watu wajue." Ninaamini kwamba kupaza sauti yako kunawasaidia wahasiriwa wengine, na kwa hatua kunajenga uwezo wa pamoja.

Kwa hivyo, kwa wale wote wanaoshughulikia usawa wa kijinsia na kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake, nawasihi pazeni sauti zenu na kupiga kelele kwa sauti kubwa kadiri muwezavyo.

Baadhi ya wanawake wanaopaza sauti zao wanakabiliwa na chuki. Je, unashughulikiaje jambo hilo?

Unapopambana na uovu, unapaswa kutarajia kukumbana na chuki. Mimi binafsi, najitayarisha kwa kupuuza chochote kinachosemwa kunihusu. Mapambano haya ni makubwa zaidi; yanahusu watu wengi, nikiwemo mimi. Wale wanaowashambulia wanawake kwa kawaida wanataka kuwanyamazisha kwa sababu wanaogopa wanawake kuwa na sauti kwenye meza ya kufanya maamuzi.

Je, umeteteaje kukomeshwa kabisa kwa unyanyasaji na dhuluma ya kingono dhidi ya watoto?

Nimehusika katika jambo hili tangu miaka yangu ya ujana. Sasa nina jukwaa kama Mama wa Taifa la Sierra Leone. Nilianzisha kampeni ya “ Wasiguzwe”, inayolenga kuwalinda wasichana wetu dhidi ya ubakaji na ndoa za mapema.

Kwa maoni yangu, ndoa za mapema ni aina ya ubakaji uliohalalishwa, kwani mara nyingi hutokea bila ridhaa ya wasichana wanaohusika, inasikitisha kuwa huwa ni kwa ridhaa ya wazazi wao.

Ili kushughulikia masuala kama vile VVU/UKIMWI, vifo vya watoto, biashara haramu ya binadamu, na fistula, lazima pia tushughulikie ubakaji na ndoa za mapema.

Umesisitiza kwa dhati kuwafungulia mashtaka wabakaji nchini Sierra Leone. Kuna mafanikio yoyote?

Ndiyo, Sierra Leone sasa ni nchi ya mfano barani Afrika. Rais wetu anaamini kuwapa wanawake fursa ya kustawi na kushiriki katika ujenzi wa taifa. Kutokana na msaada wake, sasa tuna mahakama maalumu ya uhalifu wa ngono ambayo inashughulikia kesi za ubakaji pekee. Wahalifu sasa wanaweza. Sheria hii imezuia wabakaji.

Kampeni yetu imeenea kupita miji hadi kila kona ya Sierra Leone. Tumeungwa mkono na viongozi wa dini, machifu wakuu, wataalamu wa afya, walimu na wengine wengi.

Je, umepata matokeo gani mengine kufikia sasa?

Katika miaka mitano iliyopita, tumefikia kiwango cha asilimia 69 wasichana wanaoendelea na masomo yao shuleni. Hiyo ni takwimu ambayo haijawahi kutokea hapo awali. Wasichana sasa wanafaulu katika mitihani ya umma. Tuna karibu vijana 800,000 shuleni nchini, na wasichana wengi zaidi wanaendelea na masomo shuleni kwa mwaka.

Mwaka uliopita katika vifo vya watoto wachanga na watoto nchini Sierra Leone tangu 1990.

Je, unaueleza uzoefu wako kwa Akina Mama wa Taifa wengine barani Afrika?

Ndio, tuna klabu ya Akina Mama wa Taifa wa Afrika inayojulikana kama [Muungano la Akina mama wa Taifa]. Katika miaka miwili iliyopita, tumekubaliana kwa pamoja kulenga masuala ya jinsia.

Ingawa kila mama wa taifa anaweza kushughulikia mambo mengine, wote lazima pia wape kipaumbele masuala yanayohusiana na jinsia, kama vile kuhakikisha wasichana wanaingia shuleni, kuwalinda dhidi ya ubakaji na ndoa za mapema pamoja na kuwawezesha na kuwasaidia kukabiliana ulimwengu wa leo ulio na changamoto.

Je, nchi zingine zinaweza kuiga mfano wako?

Ndio, mwongozo wetu unaweza kuigwa sana. Ni rahisi: linda watu wako, linda wanawake, watoto na walio hatarini. Inawezekana. Nia yangu ni kuwalinda wasichana wadogo dhidi ya hatari za ulimwengu. Kuna njia nyingi za kuwalinda.

Je, una ujumbe gani wa mwisho kwa wasichana wadogo barani Afrika na duniani kote?

Katika ulimwengu wa sasa, lazima uwe na ndoto na uwe na lengo. Bila kujali hali yako, ikiwa una ndoto, basi una lengo. Lenga ndoto yako na uilinde kutoka kwa wale wanaojaribu kuizima, kwa sababu maisha yako yanazingira ndoto hiyo.

Endelea kuilenga na kujitolea. Kumbuka, unapokuwa kwenye safari, unapaswa kujaribu kuwavuta wengine kuandamane nawe kwa sababu, unapokuwa na wengine, unavumilia zaidi. Unapokuwa peke yako, utachoka haraka sana.

Jocelyne Sambira
More from this author