Medali ya juu kabisa ya ulinzi wa amani kutolewa kwa mlinda amani kutoka Malawi

Get monthly
e-newsletter

Medali ya juu kabisa ya ulinzi wa amani kutolewa kwa mlinda amani kutoka Malawi

山News
By: 
Praveti Chauncy Chitete kutoka Malawi alipoteza uhai wakati akiwaokoa walinda amani wenzake nchini DRC
MONUSCO
Praveti Chauncy Chitete kutoka Malawi alipoteza uhai wakati akiwaokoa walinda amani wenzake nchini DRC.

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kumefanyika maadhimisho ya siku ya walinda amani duniani ikienda sambamba na utoaji wa nishani kwa walinda amani waliopoteza maisha wakihudumu kwenye sehemu ya mizozo. Flora Nducha na maelezo zaidi.

Tukiohilo limeongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambapo kwanza ameweka shada la maua kukumbuka walinda amani wote waliopoteza maisha tangu kuanza kwa ulinzi wa amani wa umoja huo mwaka 1948.

Ni katika tukio hilo ambapo Katibu Mkuu atatoa medali ya ujasiri wa kipekee ya Kapteni Mbaye Diagne kwa mlinda amani kutoka Malawi, Chancy Chitete of Malawi ambaye aliuawa wakati wa operesheni dhidi ya waasi wa Allied Democratic Forces, ADF huko Kivu Kaskazini ambapo alimuokoa askari kutoka Tanzania.

Medali hiyo amepokea mjane wa Chitete, Lachel Chitete Mwenechanya ambaye alikuwa pia ameongozana na mwanae na dada wa Chitete.

Akimzungumzia Chitete, Katibu Mkuu amesema kwamba,“tunatoa heshima zetu kwa Chancy CHITETE, mlinda amani raia wa Malawi ambaye wakati akihudumu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC alifariki dunia wakati akijaribu kuokoa maisha ya mlinda amani mwenzake.”

Hivyo amesema kwamba“ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni uwekezaji muhimu katika amani na usalama duniani. Hata hivyo unahitaji ahadi thabiti ya kimataifa. Na ndio maana tumezindua Hatua kwa Ajili ya Ulinzi wa Amani, mpango ambao unalenga kufanya ujumbe wa ulinzi wa amani kuwa thabiti, salama na uendane na mazingira ya siku zijazo”.

Luteni Daudi Makamba, kamanda wa kikosi cha sita cha vikosi maalum ni miongoni mwa waliokuwepo wakati wa shambulio hilo la tarehe 14 mwezi Novemba akiwa kiongozi wa kikosi maalum ambapo amesema kilichotokea..

“Kweli tulipofika maeneo ya Kididiwe tulikutana na adui tuliweza kumpiga na kumnyong’onyesha kabisa. Katika mapigano hayo makali nilipoteza askari wangu mmoja, na mwingine alipigwa risasi ya mguu na mimi mwenyewe nilipigwa risasi ya bega.”

Na je kwa tukio hilo amejifunza nini? Luteni Makamba anasema kwamba“nimejifunza katika uwanja wa medani, nidhamu, ushirikiano na umoja ni kitu cha muhimu sana.”

Utoaji wa tuzo hiyo ya Mbaye Diagne utaenda sambamba na utunuku wa medali ya Dag Hammarskjöld kwa wanajeshi, polisi na watendaji wa kiraia waliopoteza maisha wakati wa ulinzi wa amani mwaka 2018 hadi mwezi Machi mwaka huu wa 2019.

Miongonimwao ni walinda amani 5 kutoka Tanzania ambao niHalum Hassan Nandala, Yulban Nzowa Nsevilwe,Erick Masauli John waliokuwa wakihudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA.

Wengine ni Mussa Shija Machibya, Mohammed Musa Omary na Mohammed Haji Alli ambao walihudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amaninchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO

Tanzania ni nchi ya 12 kwa upelekaji wa idadi kubwa ya walinda amani kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa ambapo hadi sasa ina zaidi ya watendaji 2,300 wakihudumu Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lebabonm Sudan na Sudan Kusini.

Ingawa Umoja wa Mataifa unafanya maadhimisho hayo leo tarehe 24, maadhimisho duniani kote yatafanyika tarehe 29 mwezi Mei siku mahsusi ya walinda amani duniani.

Mada: