Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Afrika, Ahunna Eziakonwa ndiye Mkurugenzi mpya wa Ofisi ya Mkoa wa Afrika wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Programu ya Maendeleo (UNDP). Bi. Eziakonwa alikuwa amehudumu kama Mratibu wa Makazi wa Umoja wa Mataifa nchini Misri, Uganda na Lesotho. Katika mahojiano yafuatayo na Kingsley Ighobor kutoka Afrika Upya, anajadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya kiuchumi ya Afrika, ikiwemo uwezeshwaji wa wanawake na vijana na eneo la biashara huru Afrika linalotarajiwa kuanza miezi michache ijayo. Hizi hapa nukuu fupi.
Afrika Upya: Katika toleo la Hali ya uchumi wa Dunia na Matarajio ya 2018 la hivi majuzi, ukuaji wa kiuchumi wa Afrika wa 2019 umekadiriwa kuwa asilimia 3.4, ongezeko dogo la asilima 0.9 kutoka 2018. Je, mataifa yanafaa kufanya nini kuongeza kasi ya ukuaji wa kiuchumi?
Ahunna Eziakonwa: Uzalishaji wa chini ni tatizo. Kunafaa kuwa na upokezi wa uvumbuzi na teknolojia mpya ili kuongeza uzalishaji katika kilimo na biashara ndogondogo. Kilimo cha kisasa katika mataifa mengi ni cha kiwango cha chini, kwa sababu bado kinatumia njia za kale, mashine hazitumiki na sio kilimo cha biashara. Hiyo inamaanisha bado tuna nafasi kubwa hapo. Chumi za bara hili zingali telezi sana kwa bei za bidhaa katika somo la kimataifa.Ìý Kwa sababu hiyo suluhu ni kutumia njia mseto. Afrika lazima iwe na bidhaa mseto na kuongeza thamani kwa bidhaa zake za kimsingi ili kuzuia kupotea kwa ajira.
Mwaka 2003 viongozi wa Afrika walikutana Maputo, Msumbiji na kukubaliana kuwekeza angalau asilimia 10 ya bajeti zao za kitaifa katika kilimo. Ni mataifa machache yaliyotimiza makubaliano hayo. Ni kwa nini baadhi ya mataifa hayawekezi pakubwa katika sekta ya kilimo?
Miaka kumi na mitano tangu Azimio laÌý Maputo, ni mataifa saba tu—Burkina Faso, Misri, Niger, Mali, Malawi, Senegal na Zambia — yametimiza lengo hili. Kwa hakika, mataifa kama Malawi yamezidisha lengo hili huku yakifikia asilimia 21 mwaka 2013 ikilinganishwa na kiwango cha wastani cha asilimia 3.1 ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kuna masuala kadha yanayochangia uwekezaji duni katika kilimo barani Afrika. Utekelezaji wa Mpango wa Marekebisho ya Miundo barani ulipunguza fedha za kilimo; ufadhili duni wa kimataifa wa kilimo unapunguza nafasi ya sera za matumizi ya kilimo; nia duni ya kisiasa ya kuharakisha utoaji wa ruzuku kwa pembejeo, kuongeza wafanyakazi wa ugani, utafiti na miundomsingi wa vijijini na riba ya juu ya mikopo hupunguza upatikanaji wa fedha kwa wakulima wa mashamba madogo. Mageuzi ya ardhi ni muhimu ili kuzuia kugawiwa kwa mashamba kwa kusudi la kuinua mapato kutokana na mashamba makubwa. Serikali za Afrika zinapaswa kupewa nafasi kuwa na sera za kuwekeza katika kilimo na kilimo cha biashara ili kuendeleza njia tofauti za kukuza kiuchumi.
Ugawaji wa ardhi huathiri wanawake kwa kiasi kikubwa, na kuna wanawake zaidi kuliko wanaume wanaohusika katika kilimo. Je, haya ni masuala sababishi?
Hilo ni moja ya matatizo ambayo niliyokuwa nikizungumzia awali. Sheria zinapaswa kukaguliwa upya ili kurekebisha baadhi ya matatizo haya. Kama ulivyosema, katika mataifa mengine asilimia 80 ya wale wanaohusika katika shughuli za kilimo ni wanawake, lakini hawana umiliki wa ardhi, hawana haki za umiliki. Utafiti umeonyesha kuwa maendeleo ya Afrika hayatapata mageuzi pasi na kuingiza wanawake katika uchumi rasmi. Ripoti ( 2016) iligundua kwamba chumi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zimekuwa zikipoteza karibu $95 bilioni kila mwaka tangu 2010 kwa sababu ya pengo la jinsia katika soko la ajira. Wanawake tayari wako, lakini kwa kiasi kikubwa wako katika uchumi usiorasmi na usiodhibitiwa kwa sheria. Hebu waza basi kama ukiachilia nguvu, vipawa na kujitolea kwa wanawake.
Mataifa yanaweza kufanya nini hasa ili kukabiliana na hali hiyo?
Lazima tuondoe sheria zote zinazowazuia wanawake kuhusika na kujiunga katika uchumi rasmi. Wanawake wanahitaji harakati za uhamasishaji ili kuondolewa kutoka kazi za kitamaduni maadam waweze kuwa na wakati wa kuendeleza elimu yao na kuweza kushindana katika uchumi.ÌýÌý Uwekezaji halisi wa kifedha kimakusudi ili kuunga mkono elimu ya wanawake ni muhimu. Uwezeshwaji kisiasa ni muhimu pia. Tumeshuhudia mataifa kama Rwanda na Misri yakichukua mwelekeo huu. Mwelekeo huu unapaswa kuwa kote katika sekta ya umma na binafsi. Harakati za kusawazisha Usawa wa Kijinsia za UNDP, ambazo zimezinduliwa katika mataifa kama Uganda, yana lengo la kukuza usawa wa jinsia katika maeneo ya kazi.
Wanawake huwa na sifa gani za kipekee?
Naam, ukiwauliza baadhi ya Marais wa Afrika ambao wamewateua wanawake, watasema, "Wanawake hawana ufisadi sana, na unapata uwajibikaji zaidi katika matumizi ya rasilimali ukimwajiri mwanamke." Pia, wanawake ndio wanaosimamia maisha ya familia zao katika mataifa mengi. Kiongozi anayejifanyia kazi, ambaye anakumbana na hali halisi ya kila siku, anaweza kufanya maamuzi yanayopendelea maendeleo ya mwanadamu.
Kwa sasa mataifa 52 yametia saini mkataba wa makubaliano ya Eneo la Biashara Huru la Bara la Afrika (AfCFTA), lakini mataifa 18 tu yametekeleza makubaliano hayo. Afrika inaweza kupata nini kutokana na eneo la biashara huru?
Kila kitu. Sioni mustakabali wa maendeleo barani Afrika bila ushirikiano fanifu wa kikanda. Huenda ni moja ya hatua muhimu sana ambazo bara hili limechukua kushughulikia kinaya chake cha soko. Ingawa idadi ya watu Afrika ni zaidi ya bilioni 1.2 na inatarajiwa kufikia bilioni 2.5 kufikia 2050, masoko yetu ni madogo na yamegawanyika na hayana nafasi ya kushindana kimataifa yasiposhirikiana. Hivyo biashara kati ya mataifa ya Afrika itaongeza ushindani wetu kwa mujibu wa biashara ya kimataifa.
Je, Umoja wa Mataifa unafanya nini ili kuhamasisha mataifa yaliyobaki nyuma kujiunga na AfCFTA?
Umoja wa Mataifa, ukiongozwa na Kamisheni ya Uchumi ya Afrika, unalisaidia eneo la biashara huru. Shirika la UNDP linaamini kuwa mataifa yaliyobaki nyuma yanahitaji kupata habari zaidi kuhusu jinsi yatakavyoathirika ili yaweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu jinsi ya kushiriki kikamilifu katika mchakato huu.
Tueleze kuhusu kazi ya UNDP barani Afrika kwa sasa
Shirila la UNDP liko katika kila taifa la Afrika. Tunajiona kama washiriki wa mataifa katika safari zao za maendeleo. Tunasaidia jamii kujenga fursa bora za maisha, na tunasaidia vijana katika ujasiriamali na kufanya kazi na nchi kuondoa hatari kwenye mazingira ya uwekezaji. Mwaka wa 2017 tulitoa ripoti ya kwanza ya kina juu ya ukosefu wa usawa wa mapato Afrika, iliyopendekeza mkakati wa maendeleo unaoashiriwa na "Mti wa Usawa" na "matawi manne" makuuÌý - idadi ya watu, misingi ya uchumi, maendeleo ya binadamu na ukuaji. Katika miaka mitano iliyopita, jitihada zetu za kuongeza upatikanaji wa umeme zimefikia Waafrika milioni 3.35 katika jamii 3,472. Pia tunasaidia mataifa kuunda uti wa mgongo wa kisheria ili kutoa huduma na ukuaji wa uchumi. Mwishowe, tunafanya kazi na washirika wa Kiafrika kubadili taarifa za maendeleo ya bara hili na kulionyesha kama nyenzo ya ukuaji wa ulimwengu.Ìý
Je, unaweza kutaja taifa moja au mawili mlipopata mafanikio makubwa?
Hadithi nyingi za mafanikio zinakuja akilini, kama vile Enterprise Uganda, shirika lililoanzishwa na UNDP zaidi ya miaka 20 iliyopita. Shirika hili kwa sasa ni taasisi ya kujitegemea yenye uwezo wa kusaidia taasisi kukua katika biashara. Nchini Misri, UNDP ilisaidia kuanzisha ubadilishanaji wa kwanza wa bidhaa, ambao umeongezeka kuwa biashara ya mamilioni ya birr [hela za Misri] na Soko la Hisa la Ghana ni moja ya masoko bora zaidi barani Afrika.
Kutokana na tajriba yako ukifanya kazi Afrika, je, una matumaini kuhusu mustakabali wa bara hili?
Nina matumaini kwa sababu Afrika inaendelea wakati ambapo kunaÌý teknolojia mpya za kushangaza ambazo zinaweza kuharakisha ukuaji. Tazama maendeleo ya kidijitali kwa mfano; ukitaka kutengeneza kadi za vitambulisho za raia, unaweza kutumia teknolojia mara moja. Sasa kuna nafasi nyingi za kufadhili miradi ya maendeleo kuliko hapo awali. Na viongozi wengi wa Afrika sasa wana ufahamu bora wa uwezo wa Afrika.