Ajira nzuri huwa ishara muhimu kuonyesha mafanikio ya kijana. Inatoa usalama wa kifedha kwa familia yake ya baadaye na inachangia ukuaji wa uchumi wa nchi yao. Pamoja na kwamba zaidi ya nusu ya idadi kubwa ya watu Afrika iko chini ya umri wa miaka 25, mahitaji ya ajira nzuri ni makubwa.
Obiageli Ezekwesili, Makamu wa Rais wa zamani wa Benki ya Dunia, kitengo cha Afrika katika makala yake 'Ukosefu wa ajira kwa Vijana: Changamoto na Fursa katika Ukuzaji wa Uchumi' anaandika kuwa, “Barani Afrika, vijana ni 37% ya umri wa watu wanaofanya kazi, lakini 60% ya idadi hiyo haifanyi kazi. Idadi ya vijana ni kubwa sana ikilinganishwa na fursa zinazopatikana sokoni."
Nchini Kenya kwa mfano, utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Afrika uliweka kiwango cha ukosefu wa ajira cha nchi kuwa 39%, kiwango cha juu zaidi katika kanda hiyo, ikilinganishwa na 24% ya Tanzania na 18% nchini Uganda.
Mahitaji ya ajira nzuri yanatarajiwa kukua na Taasisi ya Afrika ya Sera ya Maendeleo inakadiria kuwa bara litajumuisha 29% ya watu wote wenye umri wa miaka 15 hadi 24 ifikapo 2050.
Mashirika mengine yametatua changamoto ya ajira kwa vijana kupitia ubunifu na msingi wa ushirika wa umma, wa kibinafsi na wa kiraia ambao una uwezo wa kuwa na athari kubwa kuliko kufanya kazi kivyao.
Mfano mmoja ni Mkakati wa Viongozi Vijana wa Afrika (YALI), ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) na wawakilishi wa sekta binafsi. Kwa pamoja wanaunda fursa kwa vijana wa Afrika kwa kuongeza ujuzi wa uongozi, kukuza ujasiriamali, na kuwaunganisha viongozi wachanga wa Afrika na viongozi wengine wenye ubunifu katika sekta za kibinafsi, za raia na za umma. Programu hiyo ina vituo vinne vya uongozi katika kanda ya Akraa, Ghana na Dakar, Senegali kushughulikia Afrika Magharibi, jijini Nairobi, Kenya kushughulikia Afrika Mashariki, na moja karibu na Pretoria nchini Afrika Kusini kwa kanda hiyo ndogo.
Betty Kariuki, mkurugenzi wa ushirika wa YALI, anaamini kwamba kuunda fursa kwa vijana kunawezekana ikiwa Afrika inaweza kushirikisha sekta hizo tatu - umma, kibinafsi na asasi za kiraia – ili kufanya kazi kwa pamoja.
Anatoa mfano wa kituo cha Afrika Mashariki ambacho kinafanya kazi kwa kushirikiana na MasterCard Foundation na Deloitte East Africa Ltd, ambao ndio wakala wa utekelezi, kuunda fursa za mafunzo kwa vijana Waafrika. Kituo cha Kusini mwa Afrika nacho kinashirikiana na ÌýChuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA) na Kampuni ya Dow Chemical.
Hadi sasa, zaidi ya vijana 13,000 wa Afrika wamehitimu kutoka mpango wa YALI tangu kuanzishwa kwake mnamo 2010. Uchunguzi uliofanywa na YALI mnamo 2017 katika nchi 14 za Afrika Mashariki na Kati ulionyesha kuwa 47% ya alumni imeunda wastani wa ajira 2.75 kila mmoja. Aidha, kwa kuwa wahitimu wa programu hiyo ni tofauti, fursa hizi hupatikana kwenye bara lote, na kuajiri vijana wenye tofauti za kijiografia, kitamaduni na kijamii
Nchini Uganda
Kutoka mji wa Masaka katika eneo la Buganda, Uganda, Stephen Katende mwenye umri wa miaka 28 ndiye mwanzilishi wa Kisoboka Afrika, shirika ambalo linatafuta ujumuishaji wa kifedha kwa jamii zilizotengwa nchini Uganda. Anathamini mafunzo aliyoyapata kutoka kwa YALI, ambayo yalisaidia shirika lake kuanzisha mafunzo ya biashara kwa jamii yake na kuunda fursa za kazi kwa vijana wengine 10 kama wakufunzi.
"YALI iliniandaa kukabiliana na ulimwengu wa biashara. Nilitambulishwa kwa ujasiriamali unaotokana na ubunifu ambapo biashara inaongoza katika kutatua shida, jambo ambalo shirika nililoanzisha linahitaji, "anasema Katende.
Nchini Kenya
Nchini Kenya, Kampuni ya Huduma za Usimamizi Barani Afrika (AMSCO), shirika la sekta binafsi, lilishirikiana na Kenya Commercial Bank Foundation kuunda Huduma za Maendeleo ya Biashara kwa "mpango wa 2jiajiri" unaowapa vijana wasio na ajira na wasio na elimu fursa ya kujifunza ujuzi wa kiufundi kuwasaidia kukuza biashara ndogondogo.
2jiajiri inasimamia neno Tujiajiri. Programu hiyo ina hatua mbili. (1): Kuanzisha; mafunzo ya ustadi wa ufundi na (2): Uzalishaji, ambapo washiriki wanapokea msaada wa kifedha na huduma za ukuzaji wa biashara kwa biashara zao zilizopo au mpya kwa kipindi cha miezi 12.
Lengo kuu ni kusaidia kuunda ajira na utajiri kwa vijana wapatao 50,000 wanaojihusisha na sekta isiyo rasmi Afrika Mashariki kati ya 2016-2020. Kufikia sasa, mradi wa 2jiajiri umewapa mafunzo vijana 23,000 katika ujuzi wa kiufundi na ufahamu wa kifedha katika eneo nzima.
Joshua Oigara, Mkurugenzi Mkuu wa KCB Group, anasema: "Tumejitolea kuongeza uwekezaji ili kujenga biashara ndogondogo kwa kuwa zinatoa uwezo mkubwa wa kujiajiri, sasa wataweza kupata ufadhili ambao utawaruhusu kukua na kwa hivyo kuchukua wafanyakazi wenye ujuzi. "
Mmoja kati ya waliofaidika katika 2jiajiri, Oliver Jemuge mwenye umri wa miaka 30 na ambaye kwa sasa anaajiriwa na Wakfu huo, anasema: "Ninahimiza mashirika zaidi kuungana ili kusaidia kuunda fursa kwa vijana."
"Kuwatazama wajasiriamali hawa wachanga, haswa wale ambao nimesafiri nao kuanzia hatua ya kuanzisha biashara hadi kupata ufadhili wa biashara zao, kuwaona wakikua kutoka hatua moja hadi walipofikia sasa, imebadilisha mtazamo wangu kuhusu vijana Waafrika. Wana uwezo. Wanahitaji tu mtu wa kuwashika mikono yao na kunong'oneza, 'inawezekana' na kuwasaidia kushughulikia changamoto zilizo kwenye safari yao, haswa ufadhili na ufikiaji wa soko," anasema Bwana Jemuge.
Nchini Rwanda
Mnamo 2013, Rwanda ilizindua Youth Connekt, ushirikiano wa uwezeshaji wa vijana kati ya Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na Wizara ya Vijana. Inawafundisha vijana katika ujasiriamali na ujuzi wa maendeleo kupitia kambi za kinidhamu, ambazo zimeunda karibu ajira 1,000 za kudumu na ajira za muda mfupi 2,700 kwa vijana katika muda wa miaka mitatu.
UNDP pia ina mpango wa kujenga ushirikiano na sekta binafsi, asasi za kiraia, serikali za kitaifa na kwa msaada kutoka kwa Serikali ya Denmark, kukuza mpango huo kufikia nchi zingine za Afrika.
"Kuhudhuria Youth Connekt kulinipa mtazamo wa biashara kwa kusikiliza na kujifunza kutoka kwa watoa huduma mbalimbali juu ya jinsi ya kuanza na kukuza biashara," anasema Pearl Umuhoza, mwenye umri wa miaka 28, na mwanzilishi wa Yummy and Fresh, biashara anzilishi ya vyakula vyenye afya jijini Kigali. Tangu kuzinduliwa kwa biashara yake, ameajiri wafanyikazi sita wa kudumu.
Ìý"Nimekuza biashara hii kupitia maarifa niliyopata kwa kuhudhuria programu mbalimbali za ujasiriamali, zimenisaidia sana kufikiria na kutenda kama mjasiriamali," Bi Umuhoza anaongeza.
Afrika Magharibi
Katika eneo la Afrika Magharibi, wakfu wa Tony Elumelu Foundation (TEF) ndio mpango mkubwa zaidi wa ujasiriamali wa Waafrika na umeahidi kutoa dola milioni 100 ili kutambua na kuwezesha wajasiriamali 10,000 wa Kiafrika katika kipindi cha miaka 10. Wakfu huu ulianzishwa mnamo 2015 na Elumelu, mjasiriamali na mhisani wa Nijeria. Wakfu huu umewapa wajasiriamali wachanga 7,531 mtaji usiohitaji kulipwa wa dola 5,000 kufikia sasa. Programu hiyo pia huwezesha kutolewa kwa ushauri na mafunzo ya biashara.
Mpango huo umevutia wawekezaji wengi na washirika wenye nia kama hiyo kwa mipango mbalimbali inayotekeleza, pamoja na UNDP, Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Jiraji Kelvin Tersoo anaandika kuwa, "TEF imenifungulia fursa nyingi, zaidi ya mtaji iliyonipa kuanzisha biashara yangu, imefanya nijitwike jukumu la kuwezesha watu (kwa kuwapa ushauri)." Jiraji ndiye mwanzilishi wa Agritech Hub, Nijeria, nafasi ya ubunifu kwa watengenezaji, wajasiriamali na wanaoanza, kujenga mfumo wa ekolojia wa watengenezaji anzilishi.
Bwana Tersoo anasema kwamba somo kubwa zaidi ambalo amejifunza kama mjasiriamali ni kuwa na msimamo na kushirikiana. "Kushirikiana hufanya ndoto itimie," anasema.
Ìý