Cristina Duarte kutoka Jamhuri ya Cabo Verde ndiye Mshauri Maalum Mpya wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika. Waziri wa zamani wa Fedha na Mipango katika nchi yake, anatarajia kuleta katika wajibu wake mwelekeo mpya wa kimkakati wa 'Afrika kwa Afrika' kusaidia Umoja wa Mataifa kufanikiwa barani. Katika mahojiano haya na Elizabeth Scaffidi wa Habari za Umoja wa Mataifa, Bi Duarte anaeleza maono yake na mwelekeo wa sera unaohitajika kwa maendeleo endelevu ya bara. Madondoo:
Habari za Umoja wa Mataifa: Tufahamishe kidogo kukuhusu na jinsi ulipata wadhifa huu?
Cristina Duarte: Nina tajriba ya muda mrefu katika nyadhifa za uongozi. Nilianza mapema. Nilipata fursa ya kutekeleza uongozi katika sekta ya kibinafsi, mfumo wa kifedha wa kimataifa, mashirika ya kimataifa na serikalini.
Je, nini vipaumbele vyako katika Ofisi ya Mshauri Maalum katika Umoja wa Mataifa kuhusu Afrika?
Nimekuwa katika wadhifa huu kwa karibu siku 60. Ofisi ya Mshauri Maalum kuhusu Afrika (OSAA) ni ofisi ndogo lakini yenye watu 30 walio na uwezo na mamlaka. Kama ofisi ya kimkakati, iko karibu na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Kikundi cha Afrika na watunga sera za kimkakati pamoja na wakuu barani Afrika, sio tu katika ngazi ya serikali, bali pia katika Umoja wa Afrika na ngazi ya kamisheni za uchumi za kikanda.
OSAA ina hali maalum kwa sababu ndiyo pekee katika mfumo wa Umoja wa Mataifa kuwa ofisi maalum inayohusu masuala ya kikanda, katika hali hii, masuala ya Afrika. Kwa hivyo, mchanganyiko wa rasilimali hizi zote hufanya OSAA kuweka vipaumbele vya Afrika katika mfumo wa Umoja wa Mataifa.
Afrika ina maono, mkakati wazi, na kuna mpango wa utekelezaji ambao umekuwa hatua muhimu kwa bara, hasa kwa Umoja wa Afrika. Ni muhimu kwamba mfumo wa Umoja wa Mataifa hutekeleza kile kinachopaswa kutekelezewa Afrika.
Je, baadhi ya changamoto unazotarajia ni gani?
Kila mtu amekuwa akizungumza kuhusu maendeleo endelevu na niliandika jarida miezi michache tu iliyopita ambapo nilitetea msimamo rahisi sana. Kukabiliana au kufanikiwa katika suala la maendeleo endelevu, uundaji wa sera barani Afrika unapaswa kwanza kushughulikia, kama masharti, ufadhili endelevu. Tusiposhughulikia hili, tutakuwa tukilinganisha kudhibiti umaskini na kudhibiti maendeleo. Haya ni masuala mawili tofauti. Tumekuwa tukidhibiti umaskini. Ni wakati wa Afrika kubadilika kutoka kudhibiti umaskini hadi kudhibiti maendeleo na kugeuza uundaji wa sera ipasavyo.
Uundaji wa sera barani Afrika unapaswa kujikita katika kupambana na mtiririko haramu wa kifedha, uhamasishaji wa rasilimali za ndani, na kuwafanya wafanyakazi na wananchi kiini cha sera. Kwa mfano, kujadili vikwazo vya hakimiliki ambavyo vimekuwa vikizuia Afrika kupata teknolojia na uvumbuzi, msisitizo wa anga safi, viwanda vinavyoweka mikakati kuhusu and safi, na eneo huru la biashara Afrika.
Je, COVID-19 imeathiri bara hili vipi?
Janga hili ni la dharura, sio tu katika mwelekeo wa kiafya lakini pia katika athari za kiuchumi. Kufungwa kwa shughuli, kwanza ulimwenguni na kisha katika baadhi ya nchi za Afrika, kumesukuma Afrika katika janga la kwanza la kijamii na kiuchumi katika miaka 25, wakati ambapo Afrika ilikuwa ikijiandaa kuinuka kwa mujibu wa Ajenda 2063 [ya Umoja wa Afrika].
Ingawaje barani Afrika COVID-19 imepita mipaka ya hali dharura, inajitokeza kama swala la kimaendeleo pia kwa sababu imevuruga mambo. Ninaamini kwamba, licha ya athari zake kali, COVID-19 inatoa fursa kadhaa na tunahitaji zana za kubadilisha fikira zetu ili kuzinyakua fursa hizo.
Je, matendo ya kimataifa yanawezaje kuwa na wajibu bora katika kufikia malengo ya OSAA?
OSAA sio chombo cha utendakazi kwa kila mmoja lakini ni muhimu kwa vyombo vya utendaji katika mfumo wa Umoja wa Mataifa. OSAA ni chombo muhimu katika kutoa uchanganuzi, kwa wakati unaofaa kwa masuala ya Kiafrika, kumaanisha kuwa kwa njia fulani ni chombo kinachoongozwa na mahitaji.
Tunashughulika na wadau kadhaa ndani na nje ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, ikijumuisha Umoja wa Afrika, serikali za Afrika, washirika wa kimkakati wa Afrika, n.k. Kwa hivyo, OSAA inapaswa kufanya kazi ya maana yenye athari kwa wadau. Wazo ni kuanzisha ajenda ya kimkakati ili uhusiano huu kati ya OSAA na wadau uongozwe kimkakati kwa lengo na madhumuni.
Je, kunazo hafla zozote za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa ambazo zimekusaidia kuendeleza malengo yako?
Nimekuwa hapa kwa takribam siku 60. Ndiyo kazi yangu ya kwanza katika Umoja wa Mataifa. Ninachoweza kukuambia ni kwamba licha ya kuwa hapa katika kipindi kifupi, ndani ya siku 30, nimekutana na zaidi ya mabalozi 34 wa Afrika. Tulijadili masuala kadhaa, niliwasilisha mapendekezo na walitoa maoni na kunipa ushauri. Niliwasilisha muhtasari wa dhana kwa kikundi cha Kiafrika kuhusu jinsi ya kurekebisha uhusiano wetu kupitia ajenda ya kimkakati na nikapata msaada kamili kutoka kwa kikundi cha [Afrika].
Je, kuna kitu kingine chochote ungependa kuongeza?
Leo OSAA iko katika nafasi nzuri, na itakuwa katika nafasi nzuri zaidi katika miezi michache ijayo, kumsaidia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Naibu Katibu Mkuu katika kuunda upya mwelekeo kuhusu Afrika katika mfumo wa Umoja wa Mataifa - hadithi inayotoka Afrika kwa Afrika, ambapo Malengo ya Maendeleo Endelevu yameunganishwa na Ajenda 2063 ya Afrika - pamoja na kusaidia kikundi cha Kiafrika, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD), na Kamisheni ya Umoja wa Afrika.