Eliaba Anthony Amba anaishi na mkewe na wanawe wawili katika kijiji kimoja huko Maridi, magharibu mwa Juba, jiji kuu la Sudan Kusini.
Bwana Amba, ambaye ni mkulima wa mahindi na mihogo pia ni Msaidizi wa Afya ya Nyumbani (HHP) anayeshughulikia kaya 20 zilizo na takriban watu 175. Aidha ni mlemavu, ila hilo halimzuii kuzisambaza jumbe kuhusu afya kwa watu wanaoishi katika jamii yake.
Kama msaidizi wa afya ya nyumbani aliyeidhinishwa na kijiji pamoja na chifu wa eneo lake, wajibu wa Bwana Amba ni kuwafundisha wenyeji kuhusu taratibu za kimsingi za usafi kama kuosha mikono, kula chakula chenye lishe bora na kupata chanjo. Aidha anawahimiza kina mama wajawazito kujifungulia hospitalini ili kupunguza vifo vya kina mama wanaojifungua, vya watoto na vya watoto wachanga.
Sudan Kusini ina moja kati ya viwango vya juu vya vifo vya watoto, vya watoto wachanga na kina mama wanaojifungua duniani kote, na wasaidizi wa afya wa jamii kama yeye hutekeleza jukumu muhimu katika kuimarisha uwezo wa kupata elimu kuhusu afya katika jamii.
Msaidizi wa Afya ya Nyumbani, Eliaba Anthony Amba (kulia) akizungumza na Bennet Khamis
Takwimu kutoka Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa (UNFPA) na Shirika la Afya Duniani (WHO) zaonyesha kwamba uwiano wa vifo vya kina mama wanaojifungua katika Sudan Kusini ilikuwa na uwiano wa watoto 789 kwa kila 100,000 waliozaliwa hai mwaka wa 2019, ilhali uwiano wa vifo vya watoto wa chini ya siku ishirini na nane na vya walio chini ya miaka mitano ulikuwa 39 na 96 kwa kila watoto 1,000 mtawalia, kulingana na Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF).
Mafundisho aliyopata Bwana Amba kutoka kwa mashirika kama Amref Health Africa nchini Sudan Kusini na usaidizi kutoka kwa Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Serikali Kuu ya Ujerumani (BMZ) na kampuni ya dawa and GlaxoSmithKline (GSK) yamempa yeye na wasaidizi wengine wa afya ujuzi na maarifa ya kuwaelimisha watu kuhusu hatua za kuyazuia maradhi kama vile unawaji mikono, afya bora na usafi, unyonyeshaji pekee, miongoni mwa hatua nyinginezo.
“Nimejifunza mengi kutoka kwa mafundisho haya. Tumefundishwa mikabala tofauti ya kuwasilisha jumbe kuhusu afya vilivyo kwa jamii,” anasema Bwana Amba.
Kazi yake ni wazi na inathaminiwa na jamii yake.
Bennet Khamis, baba wa watoto sita na mkulima katika eneo hilo, ameshuhudia matunda ya kazi ya Bwana Amba. Kabla ya usaidizi wake, watoto wa Bwana Bennet waliugua mara nyingi, haswa kwa malaria na kuhara. Hata hivyo, kwa kuwa sasa wana taarifa sahihi kuhusu namna ya kuyakabili maradhi kama haya, watoto hawaugui mara nyingi kama wakati huo.
“Eliaba Amba ameisaidia jamaa yangu sana. Nilikuwa nikitumia pesa nyingi mno katika kuwatibu wanangu kwa sababu walikuwa wakiugua mara nyingi. Alitutembelea na akatufunza hatua za kuchukua ili kuzuia baadhi ya maradhi haya,” alisema Bwana Bennet.
Aidha, aliifundisha jamaa ya Bennet kuhusu hatua bora za usafi.
“Alisistiza umuhimu wa kuyaweka mazingira yetu safi na kunawa mikono kabla ya kula. Watoto wetu wanadumisha usafi wa kibinafsi sasa,” alisema Bwana Bennet, huku akiongeza kuwa Bwana Amba huzungumza na familia yake yote kila anapowatembelea. “Tunaketi pamoja kama ilivyo katika shule. Nafurahia sana mafunzo yake; yeye ni mwalimu mzuri aliyeyabadilisha maisha yetu.”