‘Emoji’ niliyobuni kwa ajili ya siku ya wakimbizi inaashiria usawa na stahmala – O’Plerou

Get monthly
e-newsletter

‘Emoji’ niliyobuni kwa ajili ya siku ya wakimbizi inaashiria usawa na stahmala – O’Plerou

山News
18 June 2020
By: 
Emoji iliyoandaliwa na mbunifu wa michoro kwa kutumia kompyuta Grebet O’Plerou kutoka Cote D'Ivoire.
UNHCR Video
Emoji iliyoandaliwa na mbunifu wa michoro kwa kutumia kompyuta Grebet O’Plerou kutoka Cote D'Ivoire.

Mshindi wa tuzo kadhaa za ubinifu wa michoro kwa kompyuta ambaye amechora nembo ya siku ya wakimbizi duniani kwa mwaka huu wa 2020, Grebet O’Plerou amesema ushirikiano wake na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR katika mradi huo umemwezesha kufahamu zaidi suala la wakimbizi.

Grebet O’Plerou raia wa Côte d'Ivoire na mwenye umri wa miaka 22, amechora nembo hiyo ikiwa ni muunganisho wa vidole vya viganja vya mikono miwili, akisema kuwa alitumia rangi mbili tofauti za mikono kuonesha mshikamano, utofauti na kukubaliana utofauti, ambayo amesema ni misingi ya .

O’Plérou alijizolea sifa lukuki baada ya kuunda apu yenye vikaragosi 365 vya kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii au emoji vinavyozingatia utamaduni wa kiafrika na hivyo kubadili mtazamo wa watu kuhusu bara la Afrika ambapo kila siku ina emoji yake.

Akizungumzia emoji ya siku ya wakimbizi duniani, O’Plerou anasema, kuwa, “emoji hii inazingatia misingi na maadili ya UNHCR ambayo ni utofauti, kukubali tofauti na mshikamano. Kuwakilisha vitu hivyo, nilifikiria kuweka pamoja viganja vya mikono miwili yenye rangi tofauti na katika umbo la moyo.”

Sasa emoji hiyo inakwenda na neno #WorldRefugeeDay kwenye mtandao wa Twitter, kwa lengo la kujenga umakini wa watu kuhusu adha wanazokumbana nazo wakimbizi.

Mbunifu huyo wa michoro kwa njia ya kompyuta anaenda mbali akisema kuwa “kufanya kazi na UNHCR katika mradi huu kumenipatia fursa ya kuelewa vyema hali ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani na sasa nahisi ninaguswa zaidi kuhusu suala hili na hii inanifanya nijisikie vizuri.”

Siku ya wakimbizi duniani huadhimishwa tarehe 20 ya mwezi Juni kila mwaka na maudhui ya mwaka huu ni Kila hatua ni muhimu.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa maudhui hayo yanazingatia kuwa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 na maandamano yanayoendelea ya kupinga ubaguzi wa rangi yameonesha umuhimu wa kupigania dunia iliyo na usawa, dunia ambamo kwayo hakuna hata mtu mmoja atakayeachwa nyuma.

Mwaka huu Umoja wa Mataifa unakumbusha kuwa kila mtu, wakiwemo wakimbizi, wanaweza kuchangia katika jamii na kila hatua ni muhimu katika juhudi za kujenga dunia yenye usawa zaidi na jumuishi zaidi.