Jean-Paul Adam ni Mkurugenzi wa Teknolojia, Mabadiliko ya Tabianchi na Usimamizi wa Maliasili katika Tume Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa. Katika COP27 huko Sharm El Sheikh mnamo Novemba 2022, Bw. Adam alitetea mahitaji ya Afrika kwa bidii. Katika mahojiano haya na Kingsley Ighobor wa Afrika Upya, Bw. Adam anajadili mafanikio ya Afrika katika COP27 pamoja na masuala ambayo hayajatatuliwa hasa kuhusu hasara na uharibifu:
Ni masuala mukuu yapi kuhusu Afrika yamejitokeza katika COP27?
Ni matokeo mseto. Watu wengi wamezingatia kanuni ya ufadhili wa hasara na uharibifu. Hatupaswi kupuuza kiasi cha kichochezi hiki kwa mabadiliko kwa sababu ni utambuzi kwamba mataifa yaliyo hatarini zaidi yatahitaji ufadhili wa haraka kushughulikia udharura wa hatari ya tabianchi.
Upande wa pili ni kwamba COPs mbalimbali, ikiwa ni pamoja na COP27, zimezingatia sana mchakato.
Huku uanzishwaji wa mfuko huo ukiwa ushindi, ukweli ni kwamba rasilimali hazitakuja mara moja. Bado kuna mjadala mkubwa kuhusu jinsi utafadhiliwa na nani atalipa kwenye mfuko huo. Na masuala haya ni ya msingi kwa minajili ya njia bora ya utendakazi ambayo itaruhusu ufadhili kutiririka kwa wale wanaouhitaji zaidi.
Tumeona mafuriko nchini Nijeria na Pakistan. Tunaona ukame nchini Somalia na Upembe wa Afrika. Masuala haya yote yanagharimu maisha na mali, na hakuna utaratibu kwa sasa wa kutoa rasilimali haraka kushughulikia uhalisia wa hatari ya tabianchi kwa walio hatarini zaidi. Hiyo inahitimisha kidogo tulipo na matokeo ya COP27.
Afrika imeonyesha ari kuhusu pale inapotaka kuchukua hatua ila haina rasilimali.
Je, kwa mtazamo wa Afrika, COP27 ilikuwa fanifu au ya kukatisha tamaa?
Inategemea matarajio ya awali. Binafsi, sikuwa na matumaini kabla ya COP27 na kupitishwa kwa ufadhili kuhusu hasara na uharibifu kulikuwa mshangao wa kupendeza. Ikiwa ungeniuliza kabla ya COP27 kama tungepata, ningesema la.
Nadhani tunachukua maendeleo pale tunapoweza kuyapata.
Lazima tutambue uongozi mzuri wa wapatanishi wa Kiafrika na Urais wa COP27.
Lakini hatupaswi kuruhusu ushindi utuzuie kutoka kwa udharura wa tatizo hilo. Hatupaswi kuangukia tu katika mzunguko ule ule wa COPs zilizopita ambapo mengi kimsingi huishia katika mchakato kwa mwaka mwingine.
Kuhusu hasara na uharibifu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa [António Guterres] ametoa wito wa kutozwa ushuru kwa makampuni ya mafuta ya visukuku kimataifa. Hili linaweza kufanywa mara moja na litazalisha rasilimali kwa hasara na uharibifu kwa muda wa kimpito.
Tumeona thamani ya utetezi wa tabianchi katika ngazi ya mtu binafsi. Wapiga kura wengi kote ulimwenguni sasa wanaona mabadiliko ya tabianchi kama suala kuu, na wanasiasa wanajaribu kulishughulikia hilo. Katika hali mbaya zaidi, wanasiasa wanazitoa semi tu kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi na kujaribu kujitenga. Katika hali nzuri zaidi, wanahamia kwenye hatua halisi. Kuna thamani ya halisi kwa raia kuhakikisha kuwa serikali zinazishikilia ahadi ambazo zimetoa.
Mataifa mengi yanatazamia kuzitoza kampuni hizi ushuru kwa hazina zao, lakini tunahitaji mshikamano wa kimataifa.
Jambo jingine chanya ni kwamba niliona nia na dhamira nyingi kutoka kwa mataifa ya Kiafrika yanayotaka kutekeleza unyumbufu wa tabianchi kwa masharti yao wenyewe, kwa kuzingatia raslimali walizonazo; iwe katika suala la kupitisha njia za nishati ambazo ni nyumbufu zaidi na endelevu au kwa kweli kuwekeza katika ukabilifu wa tabianchi.
Aidha niliona kuwa mvuto kwa masoko ya mikopo ya kaboni sio tu kuhusu kuchanga fedha, ni kwa sababu pia kudai mikopo unayopaswa kuwekeza katika miradi halisi inayowanufaisha raia. Mataifa kadhaa yanaliangalia hili haswa kwa nia ya kupata faida mbili. Siyo tu kuhusu fedha unazoweza kuchanga, ni kuhusu kuelekeza raslimali kwa watu wanaozihitaji zaidi.
Kwa mtazamo wa Afrika, ni nini kinachohitajika kufanywa katika ngazi ya kikanda na kitaifa ili kubadili hatua kuhusu masuala muhimu?
Kuna dharura chache. Ya kwanza inahusu nishati kwa sababu nishati itasaidia mageuzi ya Afrika. Ninachagua neno "mageuzi" badala ya "mpito" kwa sababu nadhani katika Afrika, tunapaswa kuangalia jinsi tunavyobadili hatua, sio tu kwa kuzingatia ahadi zetu chini ya Mkataba wa Paris, lakini kinachohitajika kuzigeuza chumi za mataifa ya Afrika. Na hilo litaanza na upatikanaji wa nishati.
Tuna mataifa 24 kati ya 54 ambayo yana chini ya asilimia 50 ya watu wake wakiishi bila huduma ya umeme. Hatua ya kwanza ya kuzigeuza chumi hizi ni upatikanaji wa nishati.
Kwa mtazamo wa njia nafuu na ya moja kwa moja ya kutimiza upatikanaji wa nishati katika mataifa mengi, nishati mbadala sasa ndiyo aina nafuu zaidi ya nishati. Inabidi tuwe na uhalisia, hata hivyo, ili kushughulikia masuala ya kukatikakatika katika baadhi ya mataifa.
Baadhi ya mataifa yana nishati ya maji na mengine ya jotoardhi, lakini mkazo lazima uwe kwenye mipango ya uwekezaji ambayo ni yenye uhalisia na inayoruhusu upatikanaji wa nishati na maendeleo endelevu ya viwanda.
Hicho ndicho kipaumbele nambari moja kwa Afrika.
Jambo muhimu zaidi ambalo wananchi wanaweza kufanya ni kudai kuchukuliwa kwa hatua katika ngazi ya serikali binafsi kwa sababu inaanza kwa kuomba wachukue hatua katika muktadha wa Mkataba wa Paris.
Pili, inahusu kuelekeza uwekezaji katika ukabilifu, ambayo inaruhusu mataifa kukabiliana na unyumbufu na kuwasaidia raia kwenye mstari wa mbele wa mabadiliko ya tabianchi. Huku ni kukabiliana na mambo kama vile kilimo, uvuvi wa pwani – masuala msingi. Ni kuhusu kuhakikisha uwepo wa mikondo ya ugavi ipasavyo kuhusu uzalishaji wa chakula ndani ya bara.
Tunahitaji kuangalia jinsi tunavyoweza kutumia mihimili ya Eneo Huria la Biashara ya Bara Afrika [AfCFTA] ili kuwaunganisha vyema wazalishaji na walaji wa chakula katika bara hili na kuwa na mtindo endelevu wa uzalishaji na matumizi ya chakula unaoendana na kanuni za uchumi wa mzunguko. Hiyo itatufanya kuwa endelevu zaidi katika masuala ya tabianchi na itasaidia kuboresha vitegauchumi.
Kipengele cha tatu ni ujumuishaji wa rasilimali zinazoweza kuwekezwa ili kuunda mduara huu pepe. Inabidi kuwe na utetezi unaoendelea kwa mataifa ambayo yamesababisha uharibifu ili kuzitimiza ahadi yalizotoa chini ya Mkataba wa Paris na kutoa raslimali.
Pia kuna mengi ya kusemwa kuhusu fursa za uhamasishaji wa rasilimali za ndani na hii inajumuisha kuingia katika masoko ya mikopo ya kaboni. Inahusisha jinsi tunavyoweza kulipia deni lililopo, katika hali nyingine kusimamishwa kwa deni au kufutilia mbali deni, kulipa deni lililopo upya kwa masharti nafuu zaidi.
Pia inahusu kutumia nyenzo ibuka kama vile Dhamana ya Unyumbufu na Uendelevu (Resilience and Sustainability Trust) ya IMF na kuhamasisha fursa ya kimaendeleo—kuwa na rasilimali zaidi kupitia benki kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Kuzingatia masuala haya kutachangia katika ahadi chini ya Mkataba wa Paris na kubadilisha uchumi wa Afrika wakati uo huo.
Umetaja hivi punde kwamba kuna masuala mengi yanayoendelea katika mazungumzo ya hasara na uharibifu. Je, unafikiri masuala haya yanaweza kutatuliwa kati ya sasa na COP28?
Inawezekana. Watu ambao wamehudhuria COPs nyingi wakati mwingine huona yaliyo hasi kwa sababu tunasongwa katika mchakato. Ninadhani janga la COVID-19 na mzozo wa kijeshi nchini Ukraine umetuonyesha mapungufu ya ushirikiano wa mataifa mengi.
Kuna kiwango kikubwa cha siasa za kijiografia zinazoathiri kila uamuzi unaochukuliwa katika ngazi ya kimataifa. Hali hii inasababisha kiasi fulani cha kudumaa na baya hata zaidi, pia inasababisha ukosefu wa mshikamano. Lakini uhalisia ni kwamba kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na kwa hakika katika mwelekeo wa sasa, kila mtu hupoteza.
Hata hivyo, ninabakia na matumaini kwa sababu ni vigumu sana kupata taifa kukubaliana kuhusu jambo lolote katika mazingira haya. Mkataba wa hasara na uharibifu, hata hivyo, ni dalili kwamba ushirikiano wa mataifa mengi bado uko hai na inabidi tu kuhakikisha kwamba mchakato huo hauwi lengo.
Kwa watu ambao si wapatanishi kuhusu tabianchi na ambao si watunzi wa sera, wanapaswa kufanya nini kati ya sasa na COP28 ili kuendeleza mazungumzo kwa njia ya fanifu?
Mambo mengi. Tumeona thamani ya utetezi wa tabianchi katika ngazi ya mtu binafsi. Wapiga kura wengi kote ulimwenguni sasa wanaona mabadiliko ya tabianchi kama suala kuu, na wanasiasa wanajaribu kulishughulikia hilo. Katika hali mbaya zaidi, wanasiasa wanazitoa semi tu kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi na kujaribu kujitenga. Katika hali nzuri zaidi, wanahamia kwenye hatua halisi. Kuna thamani ya halisi kwa raia kuhakikisha kuwa serikali zinazishikilia ahadi ambazo zimetoa.
Jambo muhimu zaidi ambalo wananchi wanaweza kufanya ni kudai kuchukuliwa kwa hatua katika ngazi ya serikali binafsi kwa sababu inaanza kwa kuomba wachukue hatua katika muktadha wa Mkataba wa Paris.
Je, unaona athari yoyote barani Afrika ya uanaharakati huo wa raia?
Haswa. Bila shaka, bado kuna mengi ya kufanywa katika kuhakikisha kwamba kila mtu anaelewa kikamilifu masuala changamano na yenye mielekeo mingi kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Ninadhani sasa kuna ufahamu zaidi wa jinsi hatari ya tabianchi inavyoathiri maisha yetu ya kila siku na jinsi itaathiri mustakabali wetu. Na kuna hasira nyingi barani Afrika kwamba mataifa ya Kiafrika na raia wanachangia kidogo zaidi katika suala hili lakini wangharamika zaidi kwa athari kwenye maisha yao ya kila siku.