Wagonjwa wote hao sasa wako chini ya uangalizi. Hayo yakiendelea baadhi ya wafanyabiashara ndogo ndogo wamezungumzia kile ambacho wanakumbana nacho huku wakisihi wananchi wazingatie hatua za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Eneo la Mikocheni jijini Dar es salaam nchini Tanzania, wananchi wakiwa katika harakati za manunuzi wakati huu ambapo tayari taifa hili la Afrika Mashariki limethibitisha kuwa na wagonjwa wa virusi vya Corona.
Manunuzi yanafanyika huku baadhi wakiwa na barakoa kujikinga na Corona.
Katika viunga vya Namanga nako wilayani Kinondoni shughuli za zinaendelea za biashara na usafirishaji na kando tunakutana pia na mama lishe Binti Hassan ambaye yeye anazungumzia changamoto yao akisema kuwa,"sisi wafanya biashara wadogo wadogo tatizo letu ni moja, utoke ndio ujue kupate mkono kwenda kinywani,Nawasihi wenzangu tuwemakini kwa vile wengine wanavaamaglavu na barakoa. Hizi barakoa ata wakivaa wanazitoa kwa vile hawajazoe kwa hivyo wanatoa ili wapate hewa.Kwa hivyo naona kama hali ipo palepale."
Hata hivyo Binti Hassan amesema yeye akiwa ni mama lishe anahakikisha kuwa wateja wake wananawa mikono kwa sabuni ili kuepusha kusambaza virusi vya Corona na kwamba,"nasihi wafanyabiashara wenzangu wachukue hatua hiyo pia kuepusha ugonjwa huu."
Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni,, hadi Jumatano kulikuwepo na wagonjwa 193, 475 waliothibitishwa katika nchi 164 duniani kote, na kati yao hao 7864 wamefariki dunia.