Nyimbo za wasanii kama Diamond Platnumz na Ali Kiba zinasaidia kueneza Kiswahili DRC na kutusaidia kazi ya ulinzi wa amani

Get monthly
e-newsletter

Nyimbo za wasanii kama Diamond Platnumz na Ali Kiba zinasaidia kueneza Kiswahili DRC na kutusaidia kazi ya ulinzi wa amani

山News
7 July 2020
By: 
Kamanda wa kikosi cha Tanzania huko DRC, Luteni Kanali John Ndunguru katika mazungumzo na afisa wa jeshi la DRC, FARDC huko Beni, DRC.
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua
Kamanda wa kikosi cha Tanzania huko DRC, Luteni Kanali John Ndunguru katika mazungumzo na afisa wa jeshi la DRC, FARDC huko Beni, DRC.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, lugha ya Kiswahili imekuwa nyenzo muhimu atika kutekeleza majukumu ya ulinzi wa amani ya Umoja wa Mataifa, ikitumiwa na walinda amani wa chombo hich hususan wale wanaotoka Tanzania,sambamba na raia.

Mashuhuda wa Kiswahili na ulinzi wa amani ni walinda amani wa Tanzania wa kikundi cha 7, TANZBATT 7, cha kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, .

Meja Michael Kibira ni miongoni mwao mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini na anasema kuwa, "lugha ya kiswahili imekuwa ikiongelewa katika eneo hili la Kivu kaskazini na raia wengi kuanzia wadogo ni lugha yao ambayo wanakua nayo. Na sisi tunaitumia kama ni faida kwetu kwa sababu unapokuwa unakutana na raia wa DR Congo unakuwa uko huru kuongea naye, naye anakuamini. Unajua katika maeneo ya vita, yule ambaye ni mwathirika wa vita anakuwa ni mtu ambaye anatilia shaka kila mtu ambaye ni mgeni kwake. Hapa DR Congo tumekuwa tukifanya kazi na mataifa mbalimbali kuna Malawi, Afrika Kusini na Indonesia."

Mlinda amani huyu kutoka Tanzania anatoa mfano zaidi akisema kuwa, "kwa mfano hapa ninafanya kazi na mtu kutoka Indonesia, kwa hivyo wakikutana na mtu ambaye ni raia wa Indonesia ni tofauti kabisa na wanavyokutana na sisi kwasababu wanapokutana na mimi wanakuta kwamba sihitaji kuwa na yule msaidizi wa lugha. Mimi, ana uwezo wa kunisongelea, akaongea na mimi ni kama ndugu moja na anatambua kabisa kwamba nyinyi Tanzania ni ndugu zetu tunaongea lugha moja, tunafahamiana hata kama lugha yangu mimi wa DRC haijanyooka kama Kiswahili chenu lakini tunaelewana vizuri. Kwa hivyo mimi hapa Kamango nimeitumia kama silaha ambapo naweza nikaambiwa kitu kama akiona adui anakwambia kule rafiki usiende kuna hii na hii kwa hivyo mimi nasema hiyo ni silaha na msaaada mkubwa sana kwetu watanzania kufanya kazi hapa Congo!"

Kwa upande wake Kepteni Salum Lihega, lugha ya Kiswahili inafanikisha doria kama akifafanua kuwa, "lugha ya Kiswahili imetoa msaada mkubwa sana kwetu kwasababu imeleta urahisi sana katika kuwafikia raia na kufanya nao mazungumzo mbalimbali. Lugha ya Kiswahili imeenea na hii imepelekea kutuletea urahisi sana sisi katika kuwafikia raia kuzungumza nao kupata taarifa mbalimbali na pia sisi kujenga nao mahusiano yaliyo karibu. Kuna suala moja ambalo kwa kweli naomba nilizungumze nitoe pongezi zangu za dhati kwa wasanii wetu wa Tanzania waimbaji wa nyimbo za injili na vile vile hata waimbaji wa hizi nyimbo za kizazi kipya nao wamechangia sana katika kueneza hii lugha ya Kiswahili katika nchi hii. Utasikia nyimbo za injili kama vile za Rose Mhando, na Christina Shusho na vile vile za kizazi kipya kama vile za Diamond Platnumz na Ali kiba. Sasa hivi nikipita huko mitaani huona sisi tunapita kuzungumza nao na hasa hasa wakizisikiliza zile nyimbo na kutuona sisi wanaona kwamba sisi ndio wale ambao tumekuwa tukiziimba zile nyimbo. Kwa kweli imeleta faraja sana kwa watanzania tujidai kuwa na kiswahili tujivunie, tukitetee Kiswahili tukilinde na tujitahidi kukikuza ili kiweze kuenea na sehemu mbalimbali ukiacha hapa DRC."

Lugha ya Kiswahili inasaidia kupata taarifa kutoka kwa wananchi tunaowalinda

Walinda amani hao kutoka Tanzania wanaendelea kuelezea ni kwa vipi wakiwa wanasaka taarifa za ulinzi wa amani, lugha ya Kiswahili ni nyenzo muhimu ambapo Luteni Godfrey Mzungu anasema kuwa,"niko huku katika ulinzi wa amani katika kuongoza doria mbalimbali kwa maeneo ya DRC na nimekuwa katika hili jukumu kwa maeneo ya Beni, Mavivi lakini pia nimekuwepo katika majukumu katika sehemu moja inatiwa Matombo. Mfano mzuri, mimi katika eneo la Sake katika doria zangu najitahidi kukutana na raia wengi tunaongea lugha vizuri ni tofauti kati ya majirani wenzetu ambao wapo katika hili jukumu inaleta shida sana katika kuwasiliana na raia, inafikia kipindi mpaka wawe na mtu anayetafsiri. Lakini sisi raia wanatueleza shida zao mbalimbali tunakutana na machifu wao wanatufikishia habari mbalimbali ambazo zinasaidia kabisaa katika utendaji kazi wetu."

Kwa upande wake Sajini Nassoro Mohammed anasema kuwa , "Kiswahili kimetusaidia sana kwa ndugu zetu wacongo kuleta umoja katika DR Congo, kwa hiyo tunasaidia sana na wanapenda sana tuongee Kiswahili na wanapenda sana lugha yetu ya Kiswahili kwamba kumbe lugha ya Kiswahili ni nzuri kuliko hata lugha yao, wanasema lugha yao ni ngumu kuliko kiswahili kwa vile ni rahisi sana. Sisi kimetusaidia kuliko mataifa mengine tuliyonayo kama Bangladesh, ndugu zetu wa Malawi au Afrika Kusini. Kwa hiyo sisi wanatupenda sana hata maeneo tuliyopo sasa tunafanya kazi kwa karibu hapa tulipo kwa vile tuko karibu, tukitoka tu nje tunakutana nao kwa hiyo Kiswahili kinasaidia sana."

Je raia wanasemaje? Augustine ni mkazi wa Goma jimboni Kivu Kaskazini na anakiri kuwa Kiswahili kinawaunganisha na watanzania akisema,"Kiswahili kinatusaidia sisi wanacongo na watanzania. Ni lugha ya dunia nzima na ndio maana nasema ni lugha ya amani Afrika Mashariki kwa vile sisi sote tunaongea lugha moja. Mimi nitachanganya na kifaransa watanzania wanasema wanaongea Kiswahili sanifu lakini sisi sote tunaelewana katika mazungumzo yetu na kutafuta amani nchini Congo. Kiswahili kinaleta mahusiano kama niko hapa na mtu wa Bangladesh hawezi kunielewa lakini mtu wa kutoka Afrika Mashariki tutaelewana kwa vile sote tunazungumza Kiswahili na pia inaleta amani."