Umoja wa Mataifa umetoa dola milioni 40 kwa ajili ya kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ikabiliane na dharura za kiafya zinazokabili taifa hilo, ikiwemo ugonjwa wa Ebola na Surua.
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya dharura, OCHA, Mark Lowcock amesema fungu hilo linatoka katika mfumo mkuu wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF ambapo fedha zimetolewa punde baada ya DRC kuthibitisha mlipuko mpya wa Ebola huko Mbandaka, jimbo la Equateur lililopo kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo,
Taarifa ya OCHA iliyotolewa jijini New York, Marekani leo inasema kuwa DRC inakabiliana na mlipuko wa muda mrefu wa Ebola ambao tangu uanze tena mwezi Agosti mwaka 2018, umesababisha vifo vya watu 2,200 huko jimboni Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Bwana Lowcock anasema kuwa, "fedha za CERF zitaimarisha huduma za afya za sasa hivi DRC na kuwezesha ufuatiliaji wa manusura wa Ebola na kuanzisha mfumo wa kijamii wa ufuatiliaji, utoaji taarifa mapema na uchukuaji hatua kwenye ngazi ya jamii. Halikadhalika zitasaidia kulipia vyakula, maji, huduma za kujisafi , afya na elimu pamoja na ulinzi."
Kando mwa Ebola, DRC inakabiliana pia na majanga ya afya ikiwemo mlipuko mkubwa zaidi wa Surua, ukimbizi wa ndani, ukosefu wa usalama na janga la Corona au COVID-19 ambapo hadi tarehe 4 mwezi huu wa Juni, kumekuwepo na wagonjwa 3,494 wa COVID-19 waliothibitishwa na kati yao hao 74 wamefariki dunia.
NI kwa kuzingatia hali ya sasa DRC ambapo Bwana Lowcock anakumbusha kuwa, "kile kinachoendelea DRC inakumbusha kuwa jamii ya kimataifa haipaswi kusahau majanga ya kibinadamu ambayo yalikuwepo kabla ya janga la Corona. Iwapo tutafumbia macho maeneo kama vile DRC, watu walio hatarini ambao wamenasa kwenye mzunguko wa machungu hawatakuwa na fursa ya kukabili janga la COVID-19."
Ametoa shukrani zake kwa wahisani kwa mchango wao akiwasihi waendelee kuchangia vita dhidi ya Ebola DRC.
Kwa mwaka huu, mara kadhaa DRC imekuwa katika hatua za mwisho za kutokomeza Ebola, lakini kisha ugonjwa unaibuka tena.
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, , linapendekeza kusubiri siku 42 baada ya mgonjwa wa mwisho kupimwa kwa mara mbili na kubainika hana Ebola, kabla ya kutangaza kutokomezwa kwa ugonjwa huo.
OCHA inasema kuwa juhudi endelevu zinahitajika kuepusha kuibuka kwa magonjwa ikiwemo kujengea uwezo harakati dhidi ya Ebola wakati wa mlipuko na kuimarisha mifumo ya afya kwa mujibu wa mipango ya serikali ya huduma ya afya kwa wote.
Fedha zilizotolewa leo ni nyongeza ya fungu la dola milioni 30 zilizotolewa awali na CERF.