Kikosi cha Rwanda kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, MINUSCA kimepatia maabara ya kitaifa ya kibayologia nchini humo mashine yenye thamani ya dola 200,000 kwa ajili ya kupima ugonjwa virusi vya Corona au COVID-19.
Kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, katika makao makuu ya kikosi cha walinda amani wa Rwanda kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo,katika kliniki ya ujumbe huu iliyoanza kazi tangu tarehe 17 mwezi Februari mwaka huu, wageni walianza kwa kupimwa kiwango cha joto, moja ya dalili za Corona na kisha wageni wakaoneshwa mahali pa karantini kwa watendaji wanaowasili kutoka nje ya nchi.
Kanali Joseph Safari ni kamanda wa kikosi cha Rwanda, MINUSCA, anasema“sasa, tumenzisha pia ushirikiano kusaidia wenyeji. Tumetoka maabara ya kibayolojia ya kitaifa ambako wamefunga mashine ya kusaidia kuwapima wenyeji. Kwa sababu lengo letu kuu hapa ni ulinzi wa raia. "
Mashine hiyo imekabidhiwa maabara ya kitaifa mwezi uliopita wa Aprili na itasaidia kuongeza juhudi za Wizara ya afya CAR kubaini watu walioambukizwa virusi na pia kuzuia kuenea kwa virusi, na hivyo kuokoa maisha.
Msaada huu kutoka Rwanda, ni pamoja na mafunzo ya wataalamu 14 wa maabara, Dkt Clotaire Donatien Rafaï ni Mkurugenzi Mkuu wa Maabara ya Baiolojia ya Kitaifa, CAR,“msaada uliotolewa na serikali ya Rwanda umekuwa na mafanikio makubwa kwani umeturuhusu kuanza vipimo, tukianza kwanza na wahudumu wa afya kutoka maabara ya kliniki za biolojia,na maabara ya afya ya umma, pamoja na wafanyakazi wa MINUSCA. Alhamisi iliyopita tuliruhusiwa, kupima na kutambua kwa kiwango kikubwa. Tayari tumeshapima sampuli 293, pamoja na 6 ambazo zilithibitisha kuwepo kwa virusi vya corona na sampuli zingine zote zilizosalia hazikuwa na virusi vya Corona.”