Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi za mazingira na hali ya hewa, kama vile ukame na kuangamia kwa viumbe hai, vimbunga na uchafuzi kutokana na plastiki. Zipporah Musau wa Africa Renewal alizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, Bi Joyce Msuya kuhusu jinsi mataifa ya Afrika yanaweza kupunguza baadhi ya changamoto hizi na fursa zinazopatikana kufanya hivyo.
Ni takriban mwaka mmoja tangu ulipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa UNEP, na kwa kipindi fulani ulikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji. Umeionaje safari hii?
Nilijiunga na UNEP mnamo Agosti 2018 na imekuwa safari ya kuridhisha kwangu. Kwa kuzingatia umuhimu wa mazingira katika maendeleo─umuhimu unaotokana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs)─nimefurahi kuona jinsi Umoja wa Mataifa umekuwa ukiongoza kwa njia nyingi. Kwa mfano, hivi karibuni tumetoa Mwon wa Ulimwengu wa Mazingira 6, kuonyesha kwamba tunazidi kuhusisha mazingira na masuala mapana ya maendeleo.
Je, umepata mafanikio yapi katika kuongoza UNEP?
Mafanikio muhimu kwa kweli ni Mkutano wa Nne wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa mnamo Machi 2019 ambao ulilenga uvumbuzi unaoweza kutusaidia kufikia uzalishaji na matumizi endelevu. Baada ya mazungumzo ya siku tano, mawaziri kutoka mataifa wanachama zaidi ya 170 wa Umoja wa Mataifa waliwasilisha , wakisema ulimwengu unahitajika kuharakisha hatua kuelekea kwenye mfumo mpya wa maendeleo ili kukidhi maono yaliyowekwa katika Maendeleo Endelevu ya 2030.
Mataifa wanachama yalikubali maazimio 23 yasiyokuwa ya kisheria ambayo yanahusu changamoto kadhaa za mazingira ikiwa ni pamoja na uchumi duara wa ulimwengu; ununuzi endelevu wa umma; kushughulikia taka za chakula na kubadilishana mazoea bora juu ya suluhisho la nishati na usalama. Ikiwa mataifa yatachukua yote yaliyokubaliwa hapa na kutekeleza maazimio hayo, tunaweza kupiga hatua kubwa kuelekea mfumo mpya wa ulimwengu ambao hatutakua tena kwa kuharibu asili badala yake tutaona watu na sayari zikifanikiwa pamoja.
Nafanya kazi na watu wengi hodari - wafanyakazi wa UNEP na wengine wa familia ya Umoja wa Mataifa. Kama mwanamke kutoka Afrika Mashariki, nina tajriba ya kunyenyekeza sana kutumika katika shirika hili na kuwa katika makao makuu ya UNEP jijini Nairobi kufanya kazi kuhusu masuala ya mazingira.
Je, kunazo changamoto nyingine kubwa za mazingira zinazoikabili Afrika leo na zinaweza kushughulikiwa vipi?
Ningependa kutoa muhtasari wa changamoto kubwa zinazoikabili Afrika hivi leo katika makundi manne. Mojawapo ni athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kwa kuzingatia kwamba chumi nyingi za Afrika bado zinategemea sekta ya kilimo. Kundi la pili ni lile la upotezaji wa viumbe hai kwa sababu hii inaathiri usalama wa chakula na mazingira ya asili. La tatu ni nishati kwa kuwa chumi nyingi za Afrika zinakua haraka na zinahitaji nishati ya kutosha. Mwisho, ukiangalia mwenendo wa idadi ya watu, kuna ukuaji mkubwa katika maeneo ya miji na idadi kubwa ya watu inahamia katika sehemu za miji. Uhamiaji huu unasababisha changamoto nyingi, kama ile ya udhibiti wa taka.
Je, kuna fursa zozote barani?
Kuna fursa nyingi za kufurahisha. Baada ya Mkataba wa Paris, kulikuwa na ahadi ya ulimwengu na nia ya kisiasa kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa. Hivi sasa tunashirikiana na mataifa ya Afrika kuyasaidia kukuza mipango ya kitaifa katika kupunguza maafa na kujua namna ya kukabiliana nayo. Kuhusu mazingira, mwaka ujao kutakuwa na mkutano mkubwa wa kimataifa nchini Uchina, kwenye Mkataba wa Uhai Anuai, ukiwapa mataifa wanachama wa Afrika fursa ya kuunda ajenda ya uhai anuai ya ulimwengu kwa kuelezana mikakati mizuri na faafu inayoweza kuigwa na wengine. Afrika imejaliwa masaa mengi ya jua isiyotatizwa; tunawezaje kukuza utumiaji wa nguvu za jua na mabadiliko mengine ili kuinua uchumi wa Afrika?
UNEP imekuwa ikisukuma uchumi wa kijani kwa kupendekeza matumizi machache ya kaboni, matumizi bora ya rasilimali na sera zinazojumuisha jamii. Je, mataifa ya Afrika yanawezaje kufaidika kwa haya?
Yanafaa kushinikiza matumizi ya nishati safi. Tayari tunaona maendeleo kadhaa katika upande huo. Ukifuata kinachotokea nchini Afrika Kusini, kujaribu kuondoa sekta yake kubwa ya viwanda kutoka kwa kutegemea makaa ya mawe hadi kwa nishati safi… ni mchakato wa polepole. Mabadiliko kutoka kwa vyanzo vibaya vya nishati hadi kwa safi huchukua muda. Halafu tumepiga marufuku ukataji miti na kuweka mipango ya uchumi wa kijani. Mataifa kama vile Ethiopia, Ghana na Afrika Kusini, yanafuata mkondo huu. Inahitaji mawaziri wa mazingira kufanya kazi kwa karibu sana na mawaziri wa fedha kukuza mipango hii. UNEP inatumia jukumu lake la kuita mikutano ili kusaidia mataifa wanachama kufanya hivi.
Je, ni kwa njia zipi mataifa ya Afrika yanakabili tatizo la plastiki?
Serikali, wananchi, sekta ya kibinafsi na asasi za kiraia zote zina jukumu la kuchukua kukabili tatizo la plastiki. Kuna mambo matatu ambayo serikali za Afrika na raia wanaweza kufanya. Moja ni uongozi na nia ya kisiasa ya kubuni kanuni za kupiga marufuku matumizi ya plastiki na kukuza kuchakata tena plastiki. La pili ni watu kufanya chaguo nzuri, watoto wakiwaambia mama zao “mama, papa, tafadhali usinunue plastiki.” Chaguzi za watumiaji zinaweza kushawishi miundo ya mazingira ya plastiki. Tatu, tunahitaji kusherehekea na kuendeleza utetezi wa ndani ya taifa kama vile "Flip Flopi," uvumbuzi wa asili kutoka Kenya ambapo mashua imetengenezwa kutumia plastiki inayopatikana ufuoni pekee. Hivi karibuni, mashua hiyo ilisafiri kutoka Lamu kwenda Zanzibar kufanya uhamasisho. Mwisho ni ushirikiano na sekta ya kibinafsi. Ukiangalia mifano mizuri, maeneo ambamo plastiki ya matumizi ya mara moja imepigwa marufuku, kumekuwa na makubaliano kati ya serikali na sekta ya kibinafsi ambayo inahimizwa kutafuta njia mbadala na endelevu zaidi za kubadilisha mifuko ya plastiki. Sehemu ya jukumu la UNEP ni kuendeleza maelezo ya tajriba hii. Mataifa kadhaa barani Afrika, likiwemo taifa langu, Tanzania, na Kenya, yanatafuta jinsi yanaweza kuhifadhi mbuga za kitaifa kuendeleza sekta ya utalii na rikizi za watu. Mwishowe, tunahitaji kutafuta jinsi tunaweza kushughulikia hatari ya plastiki kwa kuanzisha uduara wa uchumi. Hapa ndipo msaada wa kujenga uwezo kwa serikali utakuwa muhimu.
Je, UNEP inasaidia vipi mataifa wanachama barani Afrika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030? Hasa, ni jinsi gani UNEP ikishirikiana na mashirika ya Afrika kama vile Umoja wa Afrika inashughulikia athari za mabadiliko ya hali ya hewa?
Msaada wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira unasaidia na kuonyesha sera za kisayansi ambazo zina uwezo wa kubadilisha uhusiano wa binadamu na mazingira. Pia tunapanga majukwaa ya kimataifa - kuanzia Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa hadi mifumo ya kifedha ya kimataifa hadi makubaliano ya mazingira ya kimataifa - hatua hiyo inachochea matendo. Na tunatetea, kwa kushirikiana na wananchi kote ulimwenguni, kuwepo kwa mabadiliko. Hatuwezi kufanya haya peke yetu kwa sababu kiwango cha changamoto ni kikubwa lakini kuna fursa kubwa za kuleta tofauti na kwa hivyo ushirikiano ni muhimu. Ili kupata utetezi wa kisiasa, tunashirikiana na Umoja wa Afrika kupitia ofisi zetu huko Addis Ababa. Tunatoa ushauri wa sera, msaada wa kiufundi na kujenga uwezo. Tunafanya kazi na NEPAD na tunazungumza na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuona jinsi tunaweza kusaidia mikakati midogo ya kikanda. Nilikuwa Cape Town, Afrika Kusini, mapema mwaka huu, na kwenye mashirika mengine ya kikanda ili kujifunza jinsi mataifa yanavyoweza kubuni mipango ya uchumi wa kijani.
Je, UNEP inawahusishaje wanawake na vijana?
Tunawahusisha katika ngazi mbalimbali kama sehemu ya mchakato wa kiserikali. Wanawake na vijana ni sehemu ya msingi ya kutekeleza mipango yetu. Kwenye UNEA 4, tulielezwa na wanaharakati wengi vijana ni kwa nini wanapoteza subira na walitaka tuchukue hatua.
Ujumbe wako kwa mataifa ya Afrika kuhusu mazingira ni upi?
Afrika ina jukumu muhimu la kutekeleza kuhusu mazingira. Changamoto hizi zote za ulimwengu zina athari kwa bara hili na kwa hivyo kuna haja ya kusikizwa sauti za Afrika katika ngazi zote kwenye vikao vya ulimwengu. Pia, kujumisha na kuweka mazingira katika shughuli zote kwenye ngazi ya taifa ni muhimu kwani kutabadilisha maoni kuwa vitendo. Ushirikiano ni muhimu: Afrika ni tofauti, lakini tunaweza kujenga juu ya tofauti hizo kupata hatua ya pamoja. Changamoto zetu haziwezi kutatuliwa kila moja. Inachukua kijiji kumlea mtoto barani Afrika; itachukua kijiji kusuluhisha shida zetu za mazingira.