Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Nosiviwe Noluthando Mapisa-Nqakula, daima hukumbuka siku alipoingia katika mkutano wa mawaziri wa usalama, huku akiwa jasiri na tayari kwa majadiliano, na kugundua kwamba wenzake, hasa wanaume, walifikiri alikuwa msaidizi wa waziri tu. Mshangao wao uliongezeka alipokalia kiti kilichotengewa waziri kutoka Afrika Kusini.
“Hisia zao zilikuwa, ‘Aha, sawa, wewe ndiye Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini?’” anakumbuka Bi. Mapisa-Nqakula katika mahojiano na Africa Renewal katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.
Bi. huyo waziri ni mpole, msemaji na mwenye haiba lakini ameimarishwa na miaka mingi ya uanaharakati uliohitaji ujasiri katika enzi ya utawala wa ubaguzi na harakati zilizomfanya kuwa mkuu wa wizara muhimu za serikali.
Nyadhifa za Uwaziri
Marais mbalimbali wa Afrika Kusini wamemteua kama waziri katika wizara tofautitofauti muhimu tangu mwaka wa 2004. Thabo Mbeki alimteua kama waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi mwaka 2004; Jacob Zuma alimteua Waziri wa Magereza mnamo 2009 na waziri wa Usalama na Wanajeshi Wastaafu mwaka wa 2012. Aliishikilia Wizara ya Ulinzi mara mbili chini ya utawala wa sasa wa Rais Cyril Ramaphosa, kwanza alipouchukua usukani kutoka kwa Bwana Zuma mwaka wa 2018, na pia Mei 2019 alipochaguliwa tena kwa awamu kamili.
Kuhusu masuala yanayohusiana na uwezeshwaji wa wanawake, msimamo thabiti wa Bi. Mapisa-Nqakula unadhihirika. “Ni sharti wanawake wachukue nafasi yao,” anasisitiza. “Wanawake hawataki kusaidiwa, wanataka kutambuliwa kwa wanayoyafanya.”
Kama wanawake katika mataifa mengine ya Afrika, wanawake wa Afrika Kusini wanakabiliwa na vizingiti vingi, zikiwemo tofauti za mapato na tamaduni zinazowabagua. Hata hivyo, Bi. Mapisa-Nqakula ana matumaini kuhusu hatua zinazochululiwa na wanawake kuelekea kuwa na usawa, akiamini kwamba ufanisi wake, licha ya vizingiti vingi, na ufanisi wa wengine kama yeye, unaweza kuanzisha mabadiliko makubwa ambayo hatimaye yatahusisha jamii nzima kijamii.
“Wanawake wa Afrika Kusini ni wakakamavu na wanafaulu. Wanawake kote ulimwenguni wanachukua nafasi yao ifaavyo,” anasema.
Maoni yake kuhusu uwezeshwaji wa wanawake ni kwamba angependa msisitizo kuwekwa kwenye uwezo wao kuliko kwenye kauli mbiu ya usawa wa kijinsia na hii ndiyo sababu anaangazia mafanikio yake.
“Kwa maoni yangu huwezi kukadiria ubora kabla ya kujaribu. Ninadhani ninastahiki heshima (ya watu wa Afrika Kusini),” anasema.
Mafanikio muhimu
Moja kati ya mafanikio muhimu ya wizara yake ni kulifanya Jeshi la Taifa la Afrika Kusini (SANDF) kuwa na mvuto kwa “wanaume na wanawake [ambao] watajiunga nalo na kupelekwa katika maeneo ya kazi. Wanawake haswa wanahimizwa kujiunga na jeshi,” anaongeza.
Waziri huyo pia anaangazia kwa makini suala la michakato ya upandishwaji vyeo katika SANDF, na anasisitiza kuwepo usawa na usawia. Kwa sasa, matokeo ni mazuri kwa kuwa kuna mameja-jenerali watano na mabregedia-jenerali 38 wanawake. “Walistahiki nyadhifa zao,” anasema. Kulikuwa na meja-jenerali mwanamke mmoja tu katika SANDF miongo miwili iliyopita.
Mojawapo wa majenerali wanawake wa sasa ni Mandisa Mfeka, rubani wa kivita wa kwanza mweusi wa taifa hilo.
“Majenerali wanajua kwamba nitapekua orodha ya upandishwaji vyeo kabla ya kuiidhinisha. Wanajua waziri atauliza swali, “Je, kuna mwanamke yeyote katika orodha? Ni jambo lenye malengo ya kisiasa, na ninawafahamisha majenerali umuhimu wa kuchukua mwelekeo huo,” anasema.
Uelewa wa kisiasa katika hali hii unatokana na historia ya Afrika Kusini. Mapambano dhidi ya—na ushindi juu ya—utawala wa ubaguzi yaligeuza uelewa wa dhana ya usawa, ikiwa ni pamoja na usawa wa rangi na kijinsia, na kuufanya hoja muhimu ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii.
Sehemu ya 9 ya katiba ya Afrika Kusini ya 1996 inahimiza usawa na kupinga ubaguzi kwa misingi ya rangi, jinsia au ulemavu. Taratibu nyingine za kisheria zinazowawezesha wanawake ni pamoja na Sheria ya Uhimizaji wa Usawa na Uzuiaji wa Ubaguzi (2000), Sheria ya Usawa katika Ajira (1998) na Sheria kuhusu Dhuluma za Kinyumbani (1998).
Kufikia Juni 2019, nusu ya mawaziri walikuwa wanawake, hivyo kuifanya Afrika Kusini kuwa moja kati ya mataifa ya Afrika (mengine ni Rwanda na Uhabeshi) yaliyotimiza usawa wa kijinsia katika baraza la mawaziri.
Vipengele vya kisheria kuhusu usawa vinampa nguvu Bi. Mapisa-Nqakula kwa sasa. “Mimi huwacha malengo ya katiba yajidhihirishe katika kazi na ruwaza ya wizara yangu,” afafanua.
Walinda usalaama kutoka Afrika Kusini
Umoja wa Mataifa unatambua walinda usalama wa Afrika Kusini kwa kujitolea kwao na huduma yao pia. Waziri anasisitiza kwamba wanajeshi wa Afrika Kusini wadumishe sifa yao nzuri wanapolinda usalama nje ya taifa lao. Kwa sasa zaidi ya walinda usalama 1,000 wa Afrika Kusini wanahudumu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchini Sudan.
Japo kuna visa vya dhuluma za kimapenzi vinavyowahusisha walinda usalama wa Afrika Kusini, kwa mfano kulikuwa na visa 10 mnamo 2018 na vinne kufikia Juni 2019, shabaha ya Bi Mapisa-Nqakula ni kufikia sifuri.
“Mimi hulichukulia hili kama suala la kibinafsi. Hata tukio moja la dhuluma za kimapenzi, hunipa mhemko,” asema.
Katika mazungumzo kuhusu dhuluma za kimapenzi kutekelezwa na vikosi vinavyolinda usalama, Waziri anaashiria hisia ambazo ni mwanamke na mama mzazi pekee anaweza kuashiria. “Jambo moja linaloweza kumwaibisha mwanamune sana ni kuulizwa na waziri wa kike, ‘Ni kwa nini ufanye hivyo? Ni kwa nini upoteze kila kitu ambacho umekuwa ukiwekeza kwa miaka mingi?’ Mbali na kuwa waziri, mimi pia ni mama.”
Wizara ya Ulinzi inachukua hatua za kuimarisha nidhamu miongoni mwa wanajeshi. “Ni lazima wanajeshi wote wa Afrika Kusini wanaoenda nje kulinda usalama wapate mafundisho kabambe kuhusu dhuluma za kijinsia. Hapana hata mwanajeshi mmoja asiyejua maana ya dhuluma za kijinsia na madhara yake,” asisitiza.
Kadhalika, mahakama za kijeshi zilizowekwa katika mataifa ambako usalama unalindwa zinaharakisha usikizwaji wa kesi za dhuluma za kijinsia. Wakosaji wanakabiliwa na adhabu kali sasa kuliko zamani: wanaweza kupoteza kazi zao na ruzuku au wapewe vifungo virefu.
Waziri amesema hivi maajuzi kwamba wanajeshi watatu walipigwa kalamu, na watapoteza ruzuku zao.
Kufikia wakati aliteuliwa waziri, Bi Mapisa-Nqakula alikuwa anafahamu taratibu za uanajeshi vizuri. Alikuwa na nafasi muhimu katika chama cha African National Congress (ANC) katika enzi ya utawala wa ubaguzi wa rangi na hili lilimwezesha kupata mafundisho ya kivita nchini Angola na katika Jamhuri ya Muungano ya Usovieti. “Niliyapokea mafunzo hayo katika miaka yangu ya ujana. Nilikuwa jasira sana zama hizo,” anakumbuka.
Siku hizi, matendo na mafanikio ya Bi. Mapisa-Nqakula yanadhihirika zaidi kuliko matarajio ya wanawake ya awali na yaliyochakaa.