Mnamo tarehe 1 Januari 2021, biashara chini ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ilianza.
Mkataba wa biashara, ambao unalenga kuunda soko moja la bidhaa na huduma na kukuza usafirishaji wa mitaji na watu kuvuka mpaka, unapaswa kukuza biashara ya ndani ya Afŕika – kwa sasa biashara hiyo ni asilimia 18 pekee – na ushirikiano wa kikanda.
Inatarajiwa pia kuwa msaada kwa sekta ya ubunifu. Wadau wakuu katika sekta ya ubunifu walisema mengi walipokutana mjini Kigali, Rwanda, mwaka wa 2019, hata kabla ya eneo huru la biashara kuzinduliwa.
"Tulitaka kuweka AfCFTA wazi," alisema Josh Nyapimbi, Mkurugenzi Mtendaji wa Nhimbe Trust, asasi ya kiraia yenye ubunifu wa Afrika iliyo na makao yake makuu nchini Zimbabwe, akiongeza kuwa sekta ya ubunifu na kitamaduni inaweza "kutumia makubaliano hayo ili kuendeleza uchumi wetu."
Vivyo hivyo, Wamkele Mene, Katibu Mkuu wa ofisi tekelezi ya AfCFTA, amesisitiza haja ya vijana kujihusisha na biashara ya mipakani kupitia sekta ya ubunifu na teknolojia. Anasema kuwa ushiriki kamili wa vijana katika eneo huru la biashara unaweza kukuza uundaji wa ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Sekta ya ubunifu barani Afrika ni pana na inajumuisha sanaa za kutazamwa na maonyesho, ufundi, sherehe za kitamaduni, upigaji picha, muziki, densi, filamu, mitindo, michezo ya video, uhuishaji wa kidijitali, uchapishaji, usanifu majengo na utangazaji wa bidhaa na huduma, kulingana Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD).
Shirika hilo linabainisha kuwa sekta hii inasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa Afrika.
"Uchumi wa ubunifu na viwanda vyake ni sekta za kimkakati ambazo, zikikuzwa, zinaweza kukuza ushindani, tija, ukuaji endelevu, uwezekano wa ajira na mauzo ya nje," anasema Pamela Coke-Hamilton, Mkurugenzi Mtendaji wa UNCTAD.
Ripoti inaeleza kuwa mkataba wa AfCFTA unaweza kuunda nafasi nyingi za ajira na ujasiriamali kwa vijana wa Afrika, ikipendekeza kuwa njia zianzishwe ili vijana wanufaike na soko moja.
Bara la Afrika ndilo bara lenye watu wachanga zaidi, likiwa na umri wa wastani wa miaka 19.8 huku asilimia 65 ya wakazi wake wakiwa chini ya miaka 25.Theluthi moja ya vijana wote duniani wanatarajiwa kuwa barani Afrika ifikapo 2050. Hata hivyo kati ya vijana milioni 7 na milioni 10 wa Afrika wanatafuta kazi kila siku.
Ahunna Eziakonwa, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kanda ya Afrika ya Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ya Afrika, aliiambia Afrika Upya mapema mwaka huu kwamba AfCFTA "ni kichocheo bora zaidi cha maendeleo barani Afrika."
Mnamo Machi 2021, Bi. Eziakonwa na Bw. Mene walitia saini ushirikiano wa kimkakati kwa niaba ya UNDP na Sekretarieti ya AfCFTA ili kukuza biashara barani Afrika. Mashirika yote mawili tena yalitoa mwezi Novemba ikisisitiza kwamba biashara huru barani Afrika inaweza kuchochea takriban mifumo 10 mipya ya thamani, ambayo mingi yake itasaidia sekta ya ubunifu.
Huduma hizi zinajumuisha huduma za fedha kwa simu na huduma za kitamaduni, burudani na utalii.
“Ubunifu ndio pesa mpya, na ni wakati wa Afrika kuvuna manufaa yake,” anathibitisha Carlos Lopes, mchumi na Katibu Mtendaji wa zamani wa Tume ya Uchumi ya Afrika.
Bw. Lopes anaeleza: "Ingawa hakuna uhaba wa vipaji katika bara, Afrika imekuwa chini katika kufaidika na [vipaji vyake]… Uwepo wa Afrika katika masoko ya kimataifa ya bidhaa na huduma za ubunifu umedumazwa na uwezo wake mdogo wa usambazaji, ukosefu wa maarifa kuhusu hakimiliki, sera na kanuni zilizopitwa na wakati, pamoja na uwekezaji mdogo katika sekta hii, haswa miundombinu.
Kushughulikia hali hii kunahitaji masuluhisho matatu, kulingana na Bi Eziakonwa. Masuluhisho hayo ni, kufahamu fursa, kuwekeza katika kuwezesha mifumo ya sera, na kuondoa vikwazo kwa usafiri.
Afrika lazima kwanza itambue thamani ya kiuchumi ya wabunifu na sekta ya utamaduni, alisema.Kufikia lengo la soko moja la Afrika kunahitaji mkakati unaolengwa na unaosaidia ujifunzaji, ukuzaji wa vipaji barani Afrika, pamoja na kulegeza kwa taratibu za kutafuta visa ili kuwawezesha Waafrika, ikijumuisha wale walio katika sekta ya ubunifu, kusafiri bila kuzuiliwa kuvuka mipaka, anapendekeza.
Sekta ya filamu ya Naijeria, kwa mfano, inachangia asilimia 1.42 (au dola bilioni 7.2) kwa Pato la Taifa, na inaajiri watu 300,000 moja kwa moja na wengine milioni moja kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Sekta ya ubunifu ya Afrika Kusini inachangia asilimia 3.6 ya ajira nchini humo.
Maadhimisho ya mwaka mmoja ya AfCFTA yanapokaribia, wahusika wakuu wa sekta hii wana matumaini kwamba mkataba wa kibiashara utakabiliana na vikwazo vingi katika sekta hii.
Jacob Maaga ni msanii wa maigizo na mtaalamu wa masuala ya fedha kutoka Kenya ambaye amekuwa akifanya kazi ya kukuza biashara barani Afrika. Anasema kuwa "mfumo wezeshi wa udhibiti unaoambatana na ulinzi wa kisheria ni muhimu kwa vijana kupata manufaa ya AfCFTA."
Nchini Afrika Kusini, mjasiriamali aliyeshinda tuzo Hannah Lavery anasema anatumai kuwa AfCFTA "itafungua mawasiliano kati ya wafanyabiashara kote barani Afrika ili tuanze kutafuta, kutengeneza na kuuza nje ya mipaka."
Masuala haya na mengine yalijadiliwa mwezi uliopita katika Maonesho ya Biashara ya Ndani ya Afrika huko Durban, Afrika Kusini, ambapo Mkutano wa Mkuu wa Creative Africa Nexus (CANEX) ulizinduliwa, ukifadhiliwa na Benki ya Uagizaji Nje ya Afrika (Afreximbank).
CANEX inalenga kusaidia sekta ya ubunifu na kitamaduni barani Afrika, na Afreximbank imeanzisha kituo cha dola milioni 500 kama mtaji wa mwanzo kwa mpango huo.
Kwa mujibu wa Rais wa Afreximbank Prof. Benedict Oramah, kusaidia sekta ya ubunifu ni hatua bora.
"Katika Afreximbank, tunaelewa kikamilifu uwezo wa sekta ya ubunifu ili kuchochea biashara ya ndani ya Afrika, kuunda mamilioni ya ajira kwa vijana wa bara hili, na kukuza kuibuka kwa mifumo ya thamani ya kitaifa na kikanda," anasema Bw. Oramah. "Pia tunajua uwezo wa wabunifu katika kuchochea maendeleo ya viwanda kwa sababu hii ni sekta inayoweza kuleta faida."