Mwakilishi wa Kudumu wa Botswana katika Umoja wa Mataifa, Balozi Collen Vixen Kelapile, ndiye Rais wa sasa wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) ambalo lina jukumu la kuratibu juhudi za Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo endelevu na kuendeleza malengo yaliyokubaliwa kimataifa. Alitwaa madaraka huku kukiwa na janga la kimataifa, janga la hali ya hewa, umaskini unaoongezeka, na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, miongoni mwa changamoto zingine. Katika Sehemu ya 2 ya mahojiano haya na Kingsley Ighobor wa Afrika Upya, Balozi?Kelapile anajadili juu ya Afrika na mabadiliko ya hali ya hewa, kushughulikia ukosefu wa usawa wa kijinsia na amani na maendeleo katika bara. Hizi hapa ni dondoo:
Sasa tuzungumze kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Af?ika inachangia kidogo sana katika utoaji wa gesi chafu lakini inaathiriwa pakubwa na janga la hali ya hewa. Je, ni ushauri gani unaweza kuwapa wawakilishi wa Afrika katika huko Glasgow mwezi huu wa Novemba?
Hilo ni swali muhimu sana. Kwa ufupi, Afrika inachangia asilimia 2 hadi 3 ya jumla ya uzalishaji wa gesi chafu duniani lakini imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga la hali ya hewa. Ndilo bara lililoathirika zaidi.
Kuhusu COP26, bara hili tayari lina tajriba nzuri ya jinsi ya kufanikiwa katika mazungumzo. Kumbuka kuwa Afrika ilitekeleza jukumu kubwa katika kupitishwa kwa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu inayojumuisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Mchakato ulianza kwa Afrika kuchukua msimamo wa pamoja. Kwa hivyo, ningeshauri kutumika kwa mtazamo kama huo kwenye COP26. Afrika inahitaji msimamo wa pamoja. Kwa kufanya hivyo, lazima pia kutafakari kuhusu faida kadhaa zinazoletwa na hatua za hali ya hewa, ikijumuisha kuwa fursa ya uwekezaji na chanzo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Haipaswi kuwa tu kulalamikia kuhusu talizo la mabadiliko ya hali ya hewa. Ndiyo, ni tatizo, lakini lazima wafanye kazi ili angalau kutumia uwezo unaoweza kupatikana kutokana na utekelezaji wa Mkataba wa Paris na SDGs.
Ukiuliza inavyoweza kufanywa, nitasema, kwanza, kwamba kuwekeza katika nishati safi kutokana na ufumbuzi wa nishati mbadala ni mfano mmoja. Watu wapatao milioni 570 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara hawana umeme kwa sasa. Nishati mbadala inakuwa suluhisho la bei nafuu la nishati, kwa hivyo mtu yeyote katika biashara anaweza kusema uwekezaji huu una maana kamili. Hivi ndivyo hali ilivyo katika sehemu nyingi za dunia, na nadhani ni vivyo hivyo katika nchi za Kiafrika ambazo zinaanza kutumia nishati safi.
Pili, Afrika inapaswa kwenda kwenye COP26 kwa nia ya kutafuta mafanikio katika kukabiliana na hali hiyo.
Tume ya Kimataifa ya Urekebishaji imegundua kuwa kila dola 1 iliyowekezwa katika urekebishaji inaweza kuleta faida ya takriban dola 4. Hii inamaana hasa ukizingatia kuwa Afrika iko katika mstari wa mbele kwa athari nyingi hasi za hali ya hewa, ikiwemo matukio ya kufadhaisha kutokana na mafuriko na ukame. Naelewa kuwa Mwafrika mmoja kati ya watatu hajashughulikiwa vya kutosha na mifumo ya tahadhari ya mapema.
Kumeendelea kuwa na mazoea yaliyokita mizizi ambayo yanazuia uwezeshaji wa wanawake, hasa barani Afrika. Je, unatuma ujumbe gani kwa viongozi wa Afrika kuhusu ukosefu wa usawa wa kijinsia katika bara hili?
Kuna aina nyingi za ukosefu wa usawa, na ukosefu wa usawa wa kijinsia ni changamoto ya kipekee. Lazima nitambue kuwa kumekuwa na maendeleo. Wakati huo huo, baadhi ya mazoea yamekuwa sehemu ya tamaduni na kuyashughulikia kunaonekana kuchukua muda mrefu kuliko unavyofaa. Mengi yanaweza kufanywa ili kuboresha hali hiyo.
Ukosefu wa usawa wa kijinsia sio tu uwezeshaji wa wanawake, pia ni nyenzo muhimu ya kubadilisha uchumi na kujenga jamii yenye haki zaidi, sawa na jumuishi.
Kwa hiyo, ujumbe wangu ni rahisi sana: tusipunguze tu mapengo yaliyopo; tunapaswa kuchukua hatua za kimakusudi kutatua suala hili kabisa. Wanawake hutoa mchango mkubwa kwa uchumi wetu lakini wanabeba mzigo mkubwa wa janga la COVID-19. Ni miongoni mwa walio hatarini zaidi kwa sababu ya hali wanayojipata kwayo - ni walezi wasiolipwa na wanaendelea kuwa wahasiriwa wa dhuluma za nyumbani, zilizoongezeka wakati wa janga hili.
Ningewahimiza viongozi wa Afrika kutilia mkazo hasa katika kuleta maendeleo yatakayolenga usawa wa kijinsia katika kufanya maamuzi na kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia.
Kitu kingine kinachoweza kufanywa ni kuchanganua data kwa sababu bila hiyo, huwezi hata kupima tatizo lenyewe, wala huwezi kupima maendeleo unayofikia. Tatizo huwa wazi wakati data inachanganuliwa kwa uwazi.
Mara nyingi kuna mazungumzo kuhusu uhusiano kati ya amani na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Je, unaweza kutueleza maoni yako kuhusu hili hasa kutokana na jukumu lako kama Rais wa ECOSOC??
Bila shaka. Mwingiliano huu umekuwa sehemu ya ajenda ya ECOSOC kwa miaka mingi, na inaendelea kuwa hivyo leo.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, nilitoa pendekezo kwa ECOSOC, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu haja ya mtazamo wa kina wa maendeleo, mizozo na changamoto za kibinadamu. Pendekezo lilijumuisha haja ya kuratibu msaada kwa nchi zilizo kwenye mizozo. ECOSOC iliunda utaratibu mwaka 2002, ambao ulikuwa ni kikundi cha ushauri wa dharura kuhusu nchi za Kiafrika zinazotoka kwenye mizozo. Wakati huo hapakuwa na Tume ya Kuleta Amani.
Kikundi hiki cha ushauri kilihamisha wajibu wake kwa Tume ya Kuleta Amani mwaka wa 2007-2008.? Mkakati huu unatusaidia kuchunguza kwa karibu zaidi jinsi mienendo ya kijamii na kiuchumi inavyoingiliana na ukosefu wa usalama wa kisiasa, na kutokana na mchakato huo tunaweza kutoa mapendekezo ya kuzingatiwa na Baraza la Usalama, ambalo ni chombo kingine kikuu cha Umoja wa Mataifa tunachofanya kazi kwa karibu nacho.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa sasa limeagiza kufanyika kwa mkutano kuhusu mpito kutoka kwa misaada hadi maendeleo. Kwa hivyo, sasa kuna jukwaa jipya, ambalo limeidhinishwa na Baraza Kuu, ambalo litatoa fursa ya kukuza ushirikiano wa maendeleo, kipengele cha kibinadamu, na pia kusaidia amani katika jamii.
Je, tunaweza kufikia ndoto ya Afrika bila vita?
Ndiyo. Kupitia Umoja wa Afrika (UA), mnamo mwaka 2013, Afrika ?ilipitisha kaulimbiu Kuzima Bunduki ifikapo 2020 (sasa imeongezwa hadi 2030). Msingi wa kuwa na Afrika isiyo na mizozo au vita ni pale bunduki zitakapozimwa.
Sasa tufanye chochote tunachoweza ili kuzima bunduki hizo. Ninaamini UA imeridhiana kuhusu mkakati wa kufikia lengo hili. Ni lazima tutekeleze yale ambayo yameridhiwa, maamuzi ya viongozi wa Afrika wenyewe kuzima bunduki. Sidhani tunapaswa kukata tamaa kuhusu hili. Ninaamini kuwa hili linaweza kufikiwa.
Kwa kuzingatia mizozo baina ya raia inayoendelea kwa sasa katika sehemu mbalimbali za Afrika, pamoja na janga la hali ya hewa na hali ya COVID-19, unafikiri nchi bado zinaweza kufikia malengo ya SDG ifikapo 2030?
Ndiyo. Niko na matumanini kwa sababu ni bora kuwa na matumanini. Tutapata nafasi ya kufikia SDGs ikiwa tutatazama hali hiyo kwa njia moja ninayoshauri tutazame mijadala ya mabadiliko ya hali ya hewa kwenye COP26; yaani, jinsi tunavyotumia tajriba ya changamoto hii kujihusisha katika njia za kuleta mageuzi zaidi za kufikia SDGs. Nina matumaini kuwa tunaweza. Ninajuwa kuwa ni matumaini ya kupita kiasi.
Nataka kugusia suala la viwango vya madeni ya nchi zetu. Najua kuna mengi yanayoendelea ili kuondolea nchi za Afrika Madeni. Kweli, baadhi ya nchi za Afrika zimepokea au zimepewa msamaha wa sehemu ya deni, kusimamishwa kulipia deni, na mataifa 20 yaliyostawi zaidi (G20).
Na ninajua kuwa kuna juhudi zinazoendelea ya kusamehewa deni kabisa nchi maskini.? Hii ni muhimu sana kwa sababu inatoa usaidizi wa fedha unaohitajika angalau kukabiliana na janga la COVID-19, ambalo ni changamoto ya dharura sana. Pia itaruhusu nchi kuunda nafasi inayohitajika ya kifedha kufanya kazi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Malengo ya Maendeleo Endelevu yalibuniwa kimakusudi kuwa na malengo makubwa, na ninaamini bado tunaweza kuyafikia.
Nadhani tukichukua mtazamo jumuishi kuleta mageuzi ya kimuundo ambayo yanahitajika ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, tunaweza kufikia kitu. Tunazungumzia mageuzi sahihi ya kijamii na kiuchumi, kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa njia tofauti, kutia juhudi ili kupunguza ukosefu wa usawa, kupanua ulinzi wa kijamii, kuongeza upatikanaji wa huduma za afya, elimu na mengine mengi.