Vijana wengi wanaharakati wa tabianchi wa Kiafrika wamewasili Sharm El Sheikh, Misri, kushirikihafla za COP27 zinazofanyika kuanzia tarehe 6-18 Novemba.
Afrika Upya ilizungumza na baadhi ya vijana hawa wa Kiafrika kuhusu kile wanachotarajia kuona kikitokea kwenye kongamano la ngazi ya juu la tabianchi.
Yoanna Milad, mwenye umri wa miaka 21, kutoka Misri, anasema kuwa anataka kuishi katika mazingira safi na salama. “Sayari yetu imo taabani, na sisi vijana ndio tutakaoteseka iwapo hatua hazitachukuliwa kuinusuru. Nataka COP27 iishie kwa makubaliano ya jinsi gani na lini tutaacha kutumia mafuta ya visukuku, na jinsi tutakavyokuwa na mabasi ya umeme barabarani. Acha mataifa yatuambie sio tu kile yanachotaka kukifanya lakini kile ambacho yamefanya kufikia sasa.”
Raia mwenzake Yoanna Salma Salah, mwenye umri wa miaka 21, anarejelea hoja iyo hiyo. Aidha, Salma angependa vijana wa Kiafrika wawe katika mstari wa mbele kutafuta suluhu ya hatari ya tabianchi. "Tunatumai kwamba wanapofanya maamuzi, wanasikiliza sauti zetu na wasiwasi wetu, ili makubaliano yoyote kutoka COP27 yapate uungwaji mkono na wengi."
Athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi ni kichocheo kikuu cha Sharon Gakii, mwanaharakati wa tabianchi mwenye umri wa miaka 24 kutoka Kenya. Kwake yeye, hili ni suala la kibinafsi. “Ninatoka Kaunti ya Kajiado, eneo kame nchini Kenya. Wazazi wangu walipoteza ng’ombe wapatao 100 kutokana na ukame, na hivi sasa hawana fedha za kutosha kuwalipia wadogo wangu karo ya shule.
“Niko hapa kufanya sauti yangu isikike. Niko hapa kumfahamisha kila mtu kuwa umefika wakati wa mataifa kuzitimiza ahadi zao kuhusu tabianchi. Kwa mfano, dola bilioni 100 zilizoahidiwa na mataifa tajiri zaidi ya mwongo mmoja uliopita ili kuyasaidia mataifai maskini katika juhudi za ukabilifu kupunguza uchafuzi bado hazijatolewa. Tuko katika mwaka wa 2022. Kwa nini?" anauliza kwa kejeli.
Suluhu zote?
Sio vijana wote wa Kiafrika wanaoamini kwamba suluhu lazima zitoke katika mataifa tajiri. Dahiru Mohammad Hashim mwenye umri wa miaka ishirini na tisa, daktari kutoka Nijeria ambaye aliacha taaluma yake na kujikita katika upandaji miti, anasema, "Suluhu zuri ni suluhu la ndani ya nchi.” Anaamini kuwa ni jukumu la serikali za kitaifa kutwaa madaraka.
"Serikali zetu zinahitaji kutuonyesha jinsi zilivyotimiza NDCs zao [Michango Iliyoamuliwa Kitaifa] ()," alisema. "Mafuriko ya kudumu katika nchi yake na ukame yamesababisha kuongezeka kwa ukosefu wa usalama".
Solani Mhango, Mmalawi anayefanya kazi nchini Msumbiji na shirika lisilo la kiserikali lafor Nature (WWF) anasema angependa kusikia mengi kuhusu hasara na uharibifu.
"Ninataka kuona ufadhili wa kifedha ukiwekwa kwa hasara na uharibifu katika Afrika kwa sababu Afrika ina mahitaji maalum na mazingira. Hatuwezi kuteseka kwa hali ambayo hatukuisababisha.”
Solani analalamika kuhusu vimbunga vinavyoikumba Msumbiji mara kwa mara. “Hapana shaka kwamba tumo taabani. Vimbunga kama vile Idai [mnamo 2019] vinaharibu ardhi yetu, na kuna haja ya mataifa makubwa, tajiri na yanayochangia uchafuzi mkuu wa mazingira kutimiza ahadi zao za $ bilioni 100 za kupunguza na ukabilifu.”