Bi. Winnie Byanyima ndiye Mkurugenzi Mkuu Mpya wa Mradi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Virusi vya Ukimwi (UNAIDS), Kitengo cha Umoja wa Mataifa kilichopatiwa wajibu wa kupambana na maambukizi ya VVU, ubaguzi na vifo vinavyohusiana na UKIMWI. Alizungumza na Zipporah Musau kutoka Africa Renewal kuhusu mwitiko wa shirika hili juu ya COVID-19 barani Afrika: Hizi hapa dondoo za mazungumzo hayo:
Wakati COVID-19 ikiendelea kuenea ulimwenguni kote, mradi wa UNAIDS unafanya nini kusaidia nchi kujiandaa vyema na kupambana na janga hili la COVID-19?
Kwanza, tunaangazia Afrika kwa sababu ndilo bara dhaifu zaidi kwa janga hili.
Kwa nini Afrika
Kwa sababu tuna mzigo mkubwa zaidi wa VVU na UKIMWI na kwa hivyo COVID-19 inatupata tukiwa katika hali ngumu kiafya na kiuchumi.
Bei ya bidhaa imepungua, na ukuaji wa uchumi unapungua. Ukusanyaji wa rasilimali za kinyumbani umekwama na misaada kwa afya imepunguka na haijakuwa ikikua. Karibu nusu ya nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zina tatizo la madeni au karibu kuingia katika tatizo hilo. Kulipa madeni kumekuwa kukichukua pesa nyingi kutoka kwa bajeti za kitaifa na bajeti ya afya inaendelea kupunguka. Katika nchi ya Zambia, kwa mfano, kati ya mwaka 2015 na 2018 ulipaji wa madeni uliongezeka kwa 760%, wakati bajeti ya afya ikipunguzwa kwa 30%. Kwa hivyo, Afrika imeonekana kuwa dhaifu.
Je, mradi wa UNAIDS unafanya nini kusaidia nchi?
Mradi wa UNAIDS uliundwa kupambana na VVU na UKIMWI ulimwenguni, lakini kazi zetu nyingi ziko Afrika. Hivi sasa, tunashuhudia maradhi tandavu mawili yanayogongana, [VVU na COVID-19], na tunaitika kwa kutoa ushauri kwa serikali kuhusu namna ya kupambana nao.
Katika nchi zisizopongua 11 Mradi wa UNAIDS unaongoza mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu jopokazi la COVID-19. Tunashauri serikali kuwa mwitikio wa COVID-19 lazima ujumuishe sekta mbalimbali kwa sababu janga hili sio la kiafya tu. Ni suala la kijamii, tabia za watu na kanuni za kijamii; mifumo ya kisheria na haki za binadamu kwa sababu inashambulia wale walio hatarini zaidi. Janga hili lina nawiri kwa misingi ya ukosefu wa usawa uliopo. Huo ndio mtazamo tulioleta katika kupambana na VVU na UKIMWI. Ukitazama tume zetu za UKIMWI za Kitaifa, zinaleta taasisi zote za serikali kupambana na VVU na UKIMWI, na wala sio wizara ya afya tu.
Pia tunashauri serikali kuweka jamii katika kitovu cha mapambano dhidi ya majanga kwa sababu lazima uanze na ushinde mashinani. Ni watu katika jamii zao ambao huunda na kuongoza na kupigania maisha yao, amri za kutoka juu hazitafanya kazi. Kuwawezesha kuongoza ndiko kutafanya kazi.
Tatu, haki za kibinadamu, unyanyapaa na ubaguzi lazima zishindwe. Tunasisitiza kuheshimu haki za binadamu. Kufungiwa kunakoendelea lazima kuheshimu haki za watu hata katika harakati za kuwazuia.
Kisha baadaye, tunaleta miundombinu yetu, maabara za VVU ambazo sasa zinatumiwa kupima COVID-19. Baadhi ya wanasayansi wetu bora wa VVU sasa wanafanya kazi kwenye timu zinazopambana na COVID-19 katika nchi mbalimbali. Kwa mfano, nchini Afrika Kusini, Prof Salim Abdool Karim na Quarraisha Abdool Karim wanaongoza wanasayansi katika kuishauri serikali, kama wafanyavyo wanasayansi wawili wa VVU wa ngazi ya juu Anthony Fauci na Deborah Birx kule Marekani.
Kufanya kazi na Umoja wa Afrika pia ni muhimu sana. Tunafanya kazi na Vituo vya Afrika vya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa barani Afrika (Africa CDC) ambapo mkurugenzi wake, Dkt. John Nkengasong, amealika UNAIDS kuwa sehemu ya ushirikiano unaolenga kuharakisha upimaji wa COVID-19. Anataka kufanya vipimo milioni 10 katika miezi minne ijayo.
Mwishowe, kutokana na yale tuliyojifunza kutokana na VVU; sisi ni sehemu ya harakati ya kupigania matibabu. Kumbuka wakati dawa za kupunguza makali ya virusi zilipovumbuliwa, watu barani Uropa na Marekani walikuwa wanazipata lakini barani Afrika, mamilioni bado walikuwa wanakufa kwa sababu bei ilikuwa juu. Ilibidi tupigane ili bei ishuke. Aidha, sisi ni sehemu ya kampeni ya asasi ya kiraia kushinikiza sheria ziwekewe kabla ya chanjo kupatikana kuwa hakimiliki itakuwa ya umma ulimwenguni kote, itasambazwa kwa haki kwa maeneo yote na kutolewa bure kwa matajiri na masikini.
Tiba ya kupunguza makali ya virusi vya ukimwi imesaidia kuokoa maisha na kuzuia maambukizi ya VVU. Je, kufungiwa kwa sasa kumeathiri usambazaji wa dawa hizo kwa watu zaidi ya milioni 23.3 ulimwenguni kote ambao wako kwenye matibabu ya VVU na ambao wengi wao wako Afrika?
Baadhi ya hatua za kufungiwa katika nchi nyingi ni kukiuka haki za watu wanaoishi na VVU, kama kunyimwa uwezo wao wa kwenda kuchukua dawa. Kwa hivyo, tunashinikiza serikali kuwapa dawa za miezi mitatu hadi sita, badala ya kuwapa za kila wiki chache. Tunaona pia ukiukwaji wa haki za binadamu za mashoga na wafanyabiashara wa ngono wakikamatwa - wakituhumiwa kueneza virusi vya korona - na waliobadilisha jinsia zao wakinyimwa chakula na huduma kwa sababu hawana kitambulisho. Tunashinikiza haki zao kwa kufanya kazi na serikali na kushirikiana na asasi za kiraia.
Je, janga hili litaathiri vipi wale wanaoishi na VVU na UKIMWI?
Kuna ushahidi kwamba tunaweza kupoteza watu wapatao 470,000. Lakini sio hivyo tu, maambukizi mapya kati ya watoto kupitia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto yanaweza kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 katika nchi zingine barani Afrika. Tunaweza kuona hatua zilizofikiwa katika mapambana na VVU na UKIMWI zikirudhishwa nyuma kwa miaka ipatayo 10.
Hiyo ni hatari. Kwa hivyo, ni muhimu kuweka ujumbe huko nje kwamba tunapaswa kuendelea na mapambano mawili, dhidi ya VVU na COVID-19. Usiachilie moja kwa nyingine.
Kuna ripoti kuwa unyanyasaji wa kijinsia unazidi kuongezeka kwa sababu wanawake wamefungiwa na wanyanyasaji wao. Je, huenda tukashuhudia kuongezeka kwa maambukizi ya VVU kwa sababu hii?
Hakika! Unyanyasaji wa kijinsia ni kichochezi kikuu cha maambukizi ya VVU, haswa kati ya vijana wasichana na wanawake wachanga. Jambo la kusikitisha ni kuwa, barani Afrika, wanawake vijana 5,400 wanaambukizwa VVU kila wiki! Kiwango cha maambukizi ya wasichana ni mara nne zaidi ya kile cha wavulana wa umri mmoja. Wanawake na wasichana wako hatarini zaidi ya kuambukizwa na yote yanachochewa na kukubali unyanyasaji wa kijinsia, utamaduni wa kukubali ubabedume mbaya; ukosefu wa elimu kamili ya kijinsia shuleni. Mazingira haya ambayo humfanya msichana kukosa usalama yamezidishwa na COVID-19.
Kwa hivyo, tena, tunatoa wito kwa serikali kutoa huduma. Jamii lazima ziwe angalifu. Kiongozi wa jamii lazima azungumze. Wakati kuna tishio, tunahitaji kuwa na makazi. Tunahitaji kuongeza huduma za afya ya uzazi ambayo imekuwa ikipunguzwa serikali zinapogawa rasilimali zao. Tunasema kuwa waitikiaji wa unyanyasaji wa kijinsia, washauri, wafanyakazi wa afya ya kijinsia na uzazi wanapaswa kuchukuliwa kuwa wafanyakazi muhimu katika mwitikio wa COVID-19, na huduma zao zidumishwe.
Je, ni mafunzo gani muhimu ambayo umejifunza na haswa barani Afrika, kutokana na mwitikio wa VVU, Kifua Kikuu, Malaria?
Funzo la kwanza ni kwamba maradhi tandavu hayafanani na maradhi mengine yoyote. Majanga hunawiri kutokana na ukosefu wa usawa katika jamii. Ili kuyashughulikia, unahitaji mtazamo wa sekta mbalimbali na serikali. Kwa mfano, unahitaji wanaepidemiolojia, wanasayansi wa kijamii, washauri wa mabadiliko ya tabia na viongozi ambao wanajua jinsi ya kushawishi jamii, wanaharakati wa haki za binadamu na mawakili wa haki za kibinadamu na wabunge. Na kisha unahitaji hela.
Hatimaye unaihitaji jamii. Katika mapambano mengi, hatuoni maoni ya jamii yakitafutwa. Na hapo ndipo tutakaposhindwa kwa sababu ikiwa watu walio mashinani hawawajibiki na kupigania maisha yao, hakuna hela kutoka juu itakayasuluhisha matatizo yao. Hakuna sheria kutoka juu zitakazotatua matatizo yao.
Unahitaji kupambana na ukosefu wa usawa. Kutoza ada, katika hospitali, kama inavyofanywa katika zaidi ya nchi 40 barani Afrika, husababisha ukosefu wa usawa. Wale wasio na pesa hawataenda kwa matibabu.
Haiwezekani kushinda maradhi tandavu bila kuziba mianya katika utoaji wa huduma ya afya. Ndio sababu tunasisitiza chanjo ambayo itapatikana kwa umma wote ulimwenguni. Watu wote wasipopatiwa chanjo hakuna aliye salama.
Kisha suala la ubaguzi na unyanyapaa. Wazo hili la kuwaona wale walioambukizwa kama wahalifu na kuunda sheria kuwakataza 'kuchafua' au 'kuambukiza wengine' halifanyi kazi. Ni muhimu sana kwamba tutumie mtazamo wa haki za binadamu, onyesha heshima na utunzaji, badala ya unyanyapaa na ubaguzi.
Je, nini changamoto za kupambana na COVID-19 barani Afrika kufikia sasa?
Kuna changamoto tatu kuu: Kwanza, tuna mifumo dhaifu ya kiafya kwa sababu hatujawekeza vya kutosha. Hatuna wafanyakazi wa kutosha wa afya, vifaa na maabara za kisayansi. Kwa hivyo, tunahitaji pesa kuwekeza katika mifumo yetu ya afya ili kupambana na janga hili na kuendelea kupambana na magonjwa mengine. Kwa upande mwingine, kazi yetu ya VVU imetupatia watu wengi wanaojitolea kwenye jamii ambao wanajua jinsi ya kupambana na maradhi tandavu.
Tunahitaji kusuluhisha suala la madeni. Tutakuwa tukipambana na athari za virusi hivi kwa miaka kadhaa kwa hivyo tunahitaji madeni yasimamishwe kwa miaka miwili au mengine yasamehewe. Lazima tuwe na kifedha ya kutumia kwenye mifumo ya afya kupambana na haya maradhi tandavu au tutakuwa taabani.
Pili, tunahitaji upimaji zaidi kwa sababu virusi sasa vimeingia katika jamii. Baadhi ya idadi ya visa vya chini tunavyoshuhudia vinaweza kuwa kwa sababu hatupimi vya kutosha. Afrika Kusini imetekeleza upimaji mwingi katika jamii, lakini nchi zingine nyingi haziwezi kumudu na kwa wale walio na hela, tuko nyuma ya foleni katika ununuzi wa vifaa vya upimaji. Tunahitaji ufikiaji wa upimaji na nia njema ya kisiasa kufanya upimaji zaidi na utafutaji wa waliotagusana, kutenga na kutibu.
Tatu, ufikiaji wa chanjo. Hivi sasa, kuna chanjo zaidi ya 170 zinazojaribiwa. Baadhi yazo ziko karibu kuthibitishwa. Zikipatikana bila ya makubaliano ya mapema kuhusu ufikiaji, sisi barani Afrika ndio tutakufa, wakati wengine wakipatiwa chanjo. Tumejifunza hili kutoka kwa tajriba ya VVU na hatupaswi kulirudia.
Nimefurahi sana kwamba Rais Ramaphosa (Afrika Kusini), Rais Nana Akufo-Addo (Ghana), Rais Macky Sall (Senegal) pamoja na wakuu wa zamani wa nchi 50 wametia sahihi barua wazi wakitaka kwamba chanjo ikigunduliwa iwe kwa manufaa ya umma wote ulimwenguni.
Je, una ushauri gani kwa watu barani Afrika katika kipindi hiki cha COVID-19?
Ushauri wangu wa kwanza ni kwa watu wanaoishi na VVU, na wale walio hatarini kwa COVID-19, wale walio na maradhi mengine kama ya mfumo wa kupumua na kisukari - kuwa mwangalifu. Zingatia ushauri kuhusu kukaa nyumbani, utii kanuni za kufungiwa, nawa mikono yako ili uwe salama kwa sababu uko hatarini.
Kwa watu wanaoishi na VVU, bado hatuna sayansi yote ya kutujuza jinsi walivyo katika hatari ya COVID-19. Lakini kile ningeshauri ni kwamba, ikiwa hujapimwa na unashuku kuwa na VVU, huu
ni wakati wa kupimwa kwa sababu kinga yako inaweza kuwa chini sana kiasi kwamba unaweza kuambukizwa virusi vya korona kwa urahisi.
Kwa watu wengine nitasema, ni kwa maslahi yetu wenyewe kukaa nyumbani iwezekanavyo na kuzingatia usafi wa kibinafsi. Lakini pia ni wakati wa kuwa jirani mwema - kuwasaidia wengine. Ikiwa una chakula na jirani yako hana, msaidie. Ikiwa mtu ni mgonjwa, wasilisha taarifa ili apewe msaada. Ni wakati wa kuungana, kuwa na fadhila kwa kila mmoja. Kuwa mwangalifu, kuwa salama, kutii kanuni, kuwa jirani mwema, saidia wengine, na tutakuwa sawa.
Nukuu ya mitandao ya Kijamii
''Tunashauri serikali kuweka jamii katika mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya maradhi tandavu kwa sababu lazima uanze na ushinde mwishowe. Ni watu katika jamii zao ambao huunda na kuongoza na kupigania maisha yao, amri za kutoka juu hazitafanya kazi. Kuwawezesha kuongoza ndiko kutafanya kazi.''