Wanafunzi nchini Kenya walipokuwa wakisubiri serikali kutangaza tarehe ya kufunguliwa shule baada ya likizo ndefu ya Aprili kwa sababu ya janga la COVID-19, waliombwa kusalia nyumbani kwa kipindi kingine cha majuma manne.
Hali ni hiyo hiyo katika mataifa mengi. Wanafunzi takriban milioni 297 barani Afrika wameathiriwa na kufungwa kwa shule kwa sababu ya janga hili.
Kufungwa kwa shule kwa sabau ya COVID-19 kimataifa kumeathiri wanafunzi bilioni 1.29 katika mataifa 186, ambayo ni asilimia 73.8 ya jumla ya wanafunzi ulimwenguni, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
“Hatujawahi kushuhudia hali ya kuvuruga masomo kwa kiasi hiki,” alisema hivi maajuzi Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Audrey Azoulay.
Licha ya changamoto kwamba ni wachache tu wanaoweza kupata huduma za mtandao, umeme na tarakilishi, maataifa yanaendeleza masomo kupitia mifumo mingine ya masomo ya mbali kama vile vipindi vya redio na runinga juu ya majukwaa ya mitandao na mitandao ya kijamii.
Masomo kupitia mitandao
Katika mataifa ya Misri, Ghana, Liberia, Nijeria, Moroko, Rwanda, Afrika Kusini na mengine, shule na vyuo kadhaa vimehamishia baadhi ya programu zao katika majukwaa ya mitandao na kuwahimiza wanafunzi kujiunga nayo.
Chuo Kikuu cha Ghana, kwa mfano, kimewapa mafunzo wahadhiri wake kuhusu namna ya kuendeleza masomo mtandaoni, huku kikijadiliana na mashirika ya mawasiliano ya simu kutoa data ya mtandao bure, ikiwa na upeo wa 5G kwa wanafunzi.
Victoria, mwenye umwri wa miaka 21 na mmoja kati ya mamilioni ya vijana walioathiriwa na kufungwa kwa shule nchini Ghana alisema, “Ninajiunga kwenye mtandao, kuhudhuria mihadhara, na kutagusana na marafiki zangu.”
Victoria aliambia UNICEF kwamba anajiepusha na maeneo yenye umati na anastahabu kusalia salama nyumbani. “Ninajribu pia kujifunza mambo mapya ambayo sijawahi kuyafanya – kujizoeza kupika, kusoma vitabu zaidi. Wakati mwingine ninacheza nikitaka, almuradi kuondoa mfadhaiko na ukinaifu wa kuwa nyumbani.”
Nchini Nijeria na Morocco, serikali zimeunda hazina za mitandaoni za vifaa vya masomo kwa walimu na wazazi, ilhali nchini Rwanda Halmashauri ya Elimu ya Rwanda imetenga tovuti maalumu ya kupiga jeki masomo na kutoa mtaala wa masomo, pamoja na mijarabu. Tovuti hiyo pia inawezesha mawasiliano kati ya walimu na wazazi.
Hata hivyo, masomo ya mtandaoni pekee hayakidhi wanafunzi wote kwa sabau ya kuunganishwa haba kwa intaneti, gharama ya juu ya data na tofauti kuu za kidijitali kati ya maeneo ya mijini na yale ya mashambani. Hili linaleta tishio la kuwacha mamilioni ya wanafunzi nyuma. UNESCO inasema kwamba asilimia 86 ya wanafunzi hawana tarakilishi nyumbani na asilimia 82 hawana huduma ya intaneti katika mataifa ya chini ya Jangwa la Sahara.
Mnamo Machi, Katika hafla ya kuzindua Muungano wa Kimataifa kwa Elimu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema: “Tunashirikiana kupata njia ya kuhakikisha kuwa watoto wote kila mahali wanaweza kuendelea na masomo yao, huku pakiwa na uangalizi maalumu wa jamii zilizo hatarini na zile zisizojiweza.
Mpango huu unaoongzwa na UNESCO na UNICEF wa mashirika ya kimataifa, mashirika ya kijamii na washirika wa sekta ya kibinafsi unakusudia kuhakikisha kuwa masoma yanaendelea. Utayasaidia mataifa kupata pesa na kutekeleza masuluhisho ya kiubunifu na faafu kimuktadha ili kufanikisha masomo ya mbali kwa kuinua mifumo inayotumia teknolojia ya juu, ya chini au isiyotumia teknolojia.
Shule za Redio
Mataifa pia yanaendelea kuimarisha masomo ya mbali kwa kutumia vyombo asili vya habari kama redio, na wakati mwingine, runinga. Uwezo wa redio kufikia idadi kubwa ya watu na kutohitaji ujuzi unarahisisha na kuharakisha matumizi yake kuliko kuunganisha jamii kwa mtandao.
Mataifa yanaharakisha uimarishaji wa programu zao za redio na runinga au kuzindua mipango mipya kwa usaidizi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kama UNICEF, UNESCO, Benki ya Dunia na mengine.
Kwa mfano, mashirika ya umma ya habari ya Ghana yamefufua vipindi katika redio na runinga kwa manufaa ya wanafunzi wa shule za upili. Programu kama hizo zinapeperushwa nchini Madagascar na Côte d’Ivoire. Nchini Senegal, juhudi za serikali zinasawiriwa katika kaulimbiu ya kuvutia: “Ecole fermée, mais cahiers ouverts,” inayomaanisha “shule imefungwa ila masomo yaendelea."
Radio Okapi, idhaa inayodhaminiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ilizindua Okapi Ecole (shule ya Okapi) – programu ya masomo ya mbali ya wanafunzi wa shule za msingi, upili na vyuo vya kiufundi inayopeperushwa mara mbili kwa siku.
Nchini Rwanda, UNICEF inashirikiana na Shirika la Habari la Rwanda kuzalisha na kupeperusha madarasa ya stadi msingi za hesabu na kusoma. UNICEF ilibainisha zaidi ya maandishi 100 ya redio kutoka ulimwenguni kote yanayolenga stadi msingi za kusoma na hesabu na yanayoweza kurakibishwa kuafikiana na mfumo wa elimu wa Rwanda. Msaada huu unatolewa nchini Malawi.
Nchini Côte d'Ivoire, UNICEF imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Elimu katika mpango wa ‘Shule nyumbani’ unaojumuisha kurekodi vipindi kwa nia ya kuvipeperusha katika runinga ya kitaifa.
Huku ukilenga kipindi baada ya COVID-19, Muungano wa Vyuo Vikuu vya Afrika (AAU) unaona fursa ya vyuo barani kuzingatia upanuzi wa “kumbi za kiteknolojia za kufundisha, kusoma na kutafiti.” Changamoto kama miundomsingi ya mitandao, bei ya data za intaneti na kuwepo kwa vifaa vya kidijitali zitatakiwa kushughulikiwa ili jambo hili liwe na ufanisi barani kote.